Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wawili wa China waliokutwa na hatia ya kuua tembo 226 adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya Sh108.7 bilioni.
Pia, imeamuru magari matatu ya washtakiwa hao yenye usajili wa namba T 317 BXG, T 777 BET na T 728 BGP pamoja na vipande 728 vya meno ya tembo walivyokutwa navyo vitaifishwe na Serikali.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha alisema katika shtaka la kushawishi askari polisi na maofisa wa wanyamapori wapokee rushwa ya Sh30.2 milioni ili wasiwapekue na kuwafikisha katika mikono ya sheria, kila mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela ama kulipa faini ya Sh1 milioni.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha aliwaachia huru washtakiwa hao katika shtaka la kukutwa na ganda la risasi.
Raia hao wawili wa China, Xu Fujie na Huang Gin waliokuwa wakitetewa na mawakili, Edward Chuwa na Nehemia Nkoko, waliadhibiwa adhabu hizo baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi tisa wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi wao.
Hakimu Mkeha alipokuwa akisoma hukumu hiyo, alisema katika shtaka la kukutwa na vipande 706 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh5.4 bilioni bila ya kuwa na kibali, kila mshtakiwa anatakiwa alipe fidia ya Sh54.35 bilioni na kwamba, iwapo watashindwa watumikie kifungo cha miaka 30 jela.
Akiendelea kuisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkeha alisema ametoa adhabu hizo kwa kuzingatia uzito wa maombi ya mawakili wa Serikali, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi na maombi ya utetezi ya kutaka wapunguziwe adhabu.
“Kwa kuzingatia hali halisi ya kesi, ushahidi, hasara ambayo Taifa imeipata kutokana na Tembo hao 226 waliopoteza maisha kwa kuuawa na washtakiwa ni wazi washtakiwa walitishia maisha ya vizazi vya tembo waliomo ndani ya mipaka ya nchi yetu,” alisema Hakimu Mkeha.
Alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwa kuwa umethibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote.
Kwa upande wa Mawakili wa Serikali, Nchimbi aliiomba Mahakama iwape adhabu kali washtakiwa hao kwa kuwa kati ya kipindi cha 2010 na Desemba 2013, jumla ya tembo 892 waliuawa nchini.
Alisema washtakiwa hao waliingia nchini 2010 hadi Novemba 2013 walipokamatwa kwa makosa hayo na kuwapo kwao rumande, matukio ya mauaji ya tembo yalipungua.
Nchimbi alibainisha kuwa washtakiwa hao waliua robo ya tembo wanaouawa hapa nchini na kwamba, kutokana na wingi wa nyara walizokutwa nazo, inaonekana wazi ni miongoni mwa vinara, wawezeshaji na wahusika wa shughuli za ujangili zinazoendelea nchini.
Alisisitiza kuomba wapewe adhabu kali kwa kuwa tembo ni miongoni mwa wanyama watano wanaoongeza mapato la Taifa kupitia utalii.
Wakili wa utetezi, Nkoko aliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu wateja wao kwa kuwa walikwisha kaa rumande miaka mitatu.
Washtakiwa hawa walikamatwa na nyara hizo za Serikali na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiendeshwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, uliwaita mashahidi tisa wakiwamo wapelelezi, majirani wa washtakiwa walioshuhudia upekuzi, maofisa kutoka polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao walitoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.
Miongoni mwa ushahidi wao, walidai kuwa Oktoba 20, 2013, walipokea taarifa kuwa kuna meno ya tembo yanasafirishwa kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwenda Dar es Salaam na yangeuzwa eneo la Biafra Kinondoni, Dar es Salaam.
Walidai kuwa Novemba 2,2013, waliona gari likiendeshwa na raia hao wa China walilifuatilia hadi kubaini shehena hizo za meno ya tembo zilipohifadhiwa.