Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Afisa Misitu Apuuza Agizo la Waziri wa JPM,Atukana Waandishi wa Habari

Mti ukiwa umekatwa karibu na hospitali ya rufa ya mkoa wa Shinyanga
******

Katika hali isiyotarajiwa afisa Misitu na Mazingira wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Emmanuel Nyamihula amelalamikiwa na kudaiwa kukiuka Agizo ya Naibu waziri wa Muungano na Mazingira Luhaga Mpina kwa kukata miti ovyo mjini Shinyanga hali ambayo imeanza kuufanya mji huo na kusababisha kuwa katika hali ya jangwa.


Mpina alitoa onyo la ukatwaji miti hiyo ovyo  alipokuwa kwenye ziara yake mkoani Shinyanga hivi karibuni na kutoa agizo kwa mtu atakayeonekana anakata miti holela akamatwe na kuchuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri Mpina pia aliagiza kila halmashauri itenge bajeti ya kupanda miti milioni moja na nusu ili kuondoa jangwa.


Malalamiko kuhusu afisa Misitu yametolewa leo na Afisa Maliasili na Mazingira mkoa wa Shinyanga Billie Edmott wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Billie alisema baada ya kuona miti ya mji huo inakatwa ovyo alimwambia afisa huyo wa Manispaa kuhusu kuacha kukiuka agizo la waziri  na kumuonya aache kukata miti kiholela lakini alimpuuza na kuendelea na zoezi hilo la kukata miti ovyo mitaani.


“Waziri Mpina alipokuwa katika ziara yake mkoani Shinyanga alipiga marufuku ukatwaji miti ovyo, lakini baadhi ya watendaji wameonekana kupuuzia suala hilo, na mimi kama afisa wa mkoa sipo Tayari kuwajibishwa kwa uzembe wa mtu, hivyo ninaandika barua kwa mkurugenzi wa manispaa kumkataa afisa huyo”,alisema Billie.


"Serikali ya sasa hivi kila mtu atavuna anachokipanda, halafu huyo afisa Misitu na Mazingira inasemekana siyo taaluma yake, yeye amesomea masuala ya ufugaji nyuki ndiyo maana anatuborongea utendaji kazi wetu, sisi tunataka Shinyanga iwe na miti mingi yeye anaikata ovyo sitokubaliana naye”,aliongeza Billie.



Kuhusu agizo la kila halmashauri za mkoa wa Shinyanga kutenga bajeti ya fedha ya upandaji miti,Billie alisema  limeshatekelezwa na  wanatarajia kupata fedha kwa ajili ya kuanza kununua miche na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuhifadhi mazingira.


Hata hivyo afisa huyo wa Misitu na Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga Emmanuel Nyamihula alipotafutwa na waandishi wa habari ili kuzungumzia juu ya tuhuma zinazomkabili kuhusu kupuuza agizo la waziri Mpina aligeuka mbogo na kuwatolea lugha chafu waandishi wa habari na kudai hana muda wa kuzungumza na waandishi wa habari kwani hiyo ni taaluma yake hapaswi kuingiliwa.
"Mimi huwa sitoi habari ovyo ovyo,yaani hata kama mngefanya nini siwezi kuongea na nyinyi,..hizi mnazotafuta ni habari za umbea,andikeni mnachofikiri wala msinibabaishe ..nyinyi waandishi ni wapuuzi tu msiniletee habari za umbea ",alifoka afisa misitu huyo,baadhi ya maneno hatujayaandika.
 Na Marco Maduhu-Malunde1 blog
Moja ya eneo lililokatwa miti karibu na hospitali ya mkoa wa Shinyanga

Mkazi wa Shinyanga mjini akikata kuni zinazotokana na miti iliyokatwa na afisa misitu wa manispaa ya Shinyanga-Picha na Marco Maduhu-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com