Ajali nyingi za bodaboda na mabasi ya abiria zimetajwa kuwa sababu kubwa za Taasisi ya Mifupa (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuelemewa wagonjwa wengi wanaofikishwa kwa ajili ya upasuaji wa dharura.
Hali hiyo imesababisha changamoto kubwa kwa Wizara ya Afya kwani madaktari waliopo katika taasisi hiyo ni wachache na wanazidiwa na majukumu.
Kutokana na changamoto hiyo, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema atahakikisha anashirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kutatua tatizo la kukithiri kwa ajali za bodaboda ili kupunguza mzigo mzito unaoikabili MOI kwa sasa.
Hii itakuwa mara ya pili kuweka mkakati wa kuona uwezekanao bodaboda kutumika bila ya kusababisha maafa.
Mwaka 2014 Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dares Salaam na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra) Kanda ya Mashariki walizuia bodaboda na bajaji kuingia katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, kampeni hiyo haikufanikiwa.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kozi ya wiki moja ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu inayofanyika hapa nchini kwa ushirikiano baina ya MOI na Taasisi ya Mifupa ya Chuo Kikuu cha Weil Cornel kutoka New York, Marekani, Ummy alisema asilimia 75 ya wagonjwa wanaofikishwa MOI ni kutokana na ajali za bodaboda na mabasi ya abiria.
“Tumeelezwa kwamba kati ya wagonjwa 50 wanaofikishwa MOI, asilimia 75 ni wa ajali za bodaboda na mabasi ya abiria.
Hii ni changamoto kwetu. MOI walikuwa wanapokea wagonjwa 20 kwa siku, lakini kwa sasa wanapokea wagonjwa 50,” alisema Ummy.
“Kwa hiyo, hii inaleta uzito na mzigo mkubwa kwa sekta ya afya katika kutoa huduma za afya ikiwamo upasuaji huu.
Nitaongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ana dhamana ya kuhakikisha hii biashara ya bodaboda inaendeshwa bila kuleta madhara makubwa kwa jamii.”
Kuhusu madaktari, Ummy alisema taasisi hiyo inakabiliwa na uchache wa madaktari bingwa wa upasuaji wa ubonMOI go na mishipa ya fahamu, kwani mpaka sasa kuna madaktari wanane pekee nchi nzima; mmoja yupo Hospitali ya Bugando na saba wako MOI.
“Kubwa tunalojifunza hawa ambao ni wachache wataweza kujengewa uwezo ili kuweza kujua changamoto na mahitaji ya sasa katika kufanya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, na serikali tumeahidi tutaongeza wataalamu katika fani hiyo na kununua vifaa vya kisasa vya CT Scan na MRI ili kuwaongezea ufanisi,” alisema Ummy.
Pia, alisema ametoa maelekezo kwa taasisi ya MOI kuhakikisha inasomesha wataalamu wengi zaidi.
“Nipo tayari hata kutoa maelekezo kwamba katika zile nafasi ambazo wizara inasomesha madaktari kwenda nje ya nchi, basi tuongeze wale ambao wanasomea kozi hii na watakapokuja kuanza kazi mshahara wao utakuwa mkubwa wasianze na mshahara mdogo.”
Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk Othman Kiloloma alisema tayari wameshaanza kuyafanyia kazi maagizo ya Waziri kwa kupanga ratiba za kwenda kufanya upasuaji mikoani kwa wenye uhitaji.
“Aprili 25 timu ya madaktari 10 itaondoka kwenda mikoa mitano, itaanza na Mwanza siku nne, Shinyanga tatu, Singida nne, Dodoma nne, Morogoro siku tatu na baada ya wiki mbili tutaondoka tena kwenda mikoa mingine kuanzia Bukoba mpaka Mbeya. Tutatoa taarifa kadri tunavyoendelea,” alisema Dk Kiloloma.