Hatimaye taarifa ya utekelezaji wa mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises, iliyoshinda zabuni mwaka 2011 ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37, umetua ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuanza kujadiliwa.
Akizungumza jana bungeni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo, ilifikishwa bungeni juzi na jana asubuhi wamepewa na wakaanza kuujadili papo hapo.
“Wametuletea taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo leo asubuhi (jana), ila taarifa hiyo ilifika bungeni jana (juzi), na sisi kamati tumekaa asubuhi kuijadili kama tulivyokubaliana wakati wa vikao vya kamati mjini Dar es Salaam na tutatoa taarifa ya maamuzi ya kamati,” alisema Aeshi ambaye ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini.
Akizungumza baada ya kuahirisha kikao cha kamati hiyo jana jioni, Aeshi alisema hawajafikia maamuzi na kwamba leo wataendelea kujadili taarifa hiyo na mchana watatoa maazimio ya kamati.
“Tumeahirisha kikao hadi kesho (leo) na bado tunapitia taarifa hiyo na kama kamati itaona haja ya kuwaita tena jeshi hilo kutoa maelezo, tutajua baada ya kufikia maamuzi,” alisema Aeshi na kuongeza kuwa kwa sasa wanachambua taarifa hiyo na iwapo wataona kuna haja pia ya kuutaka mkataba huo watatoa maelekezo.
Awali, Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam, kamati hiyo ilitoa siku saba kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini, kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga mashine 108 katika vituo tajwa nchini, ila hadi sasa ni vituo 14 tu ndivyo vilivyofungwa mashine hizo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainika kuwa na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.
Ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni pamoja na kampuni hiyo kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye thamani ya Sh bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.
“Ukiangalia kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,” alisema Aeshi wakati wa vikao vya Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya maagizo hayo, taarifa hiyo ya utekelezaji haikuwasilishwa kwenye kamati hiyo ndani ya muda uliokubaliwa na Aeshi alisema siku zote wamekuwa wakitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi zimekuwa zikitekeleza.
Aliongeza ila hilo la mkataba wa Lugumi lilikuwa tabu kutekelezwa hadi kamati hiyo, ilipochukua hatua za kukumbushia kwa kuandika maelezo.
Hata hivyo, baada ya taarifa za mkataba huo,zilisambaa habari kwenye vyombo vya habari kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), Said Lugumi na vigogo wengine.
Kutokana na sakata hilo, mbunge huyo alikanusha kuhusika kwake na kusema ni kweli kwamba ana urafiki wa kawaida na Said Lugumi na kusisitiza kwamba hahusiki kwa njia yoyote na kampuni hiyo.
“Kwanza kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.
Social Plugin