Bunge Labana Matumizi na Kuokoa Bilioni 6,Rais Magufuli Azungumza



Rais Magufuli ameipongeza ofisi ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 6, ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule na amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.


Ameagiza fedha hizo zipelekwe Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 120,000 ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.


Hundi Kifani ya fedha hizo imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi hicho cha shilingi Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi kifupi cha takribani nusu mwaka.


Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo Bunge limebana matumizi kuwa ni Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya nchi, Machapisho na ununuzi wa majarida, Shajala, Chakula na Viburudisho, Mtandao, Malazi hotelini, Matibabu ya wabunge na familia zao nje ya nchi, Umeme, Maji, Simu na Uendeshaji wa Mitambo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pia ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anne Kilango Malecela na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.


Rais Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 11 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea hundi kifani ya shilingi Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.


Dkt. Magufuli ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.


“Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?” Amesisitiza Rais Magufuli


Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.


Pamoja na hatua hiyo, Dkt. Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.


Katikati ya Mwezi Machi, 2016 Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 walibanika.


Kati ya shilingi Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-11 Aprili, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post