CCM WAMLIPUA LOWASSA BAADA YA KUPONDA UONGOZI WA RAIS MAGUFULI



Aliyekuwa mgombea Urais wa UKAWA kupitia CHADEMA, Ndugu Edward Lowassa, Aprili 7, 2016 alifanya mazungumzo na Wanazuoni kutoka katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.


Katika mazungumzo hayo, Ndugu Lowasa aligusia masuala mbalimbali ya Kitaifa yakiwemo hali ya siasa nchini, kuachisha kazi watumishi wenye tuhuma mbalimbali, na kile alichokiita tatizo la mfumo nchini.


Alichokifanya Ndugu Lowassa ni kutaka kuwaaminisha Watanzania masuala yasiyo sahihi kwa maslahi ya kisiasa, kwani ukweli ni kwamba; Mosi, Rais John Pombe Magufuli hatafuti umaarufu, badala yake yeye na Serikali yake wanachapa kazi ili kuwaletea maendeleo Watanzania kwa ujumla.


Pili, kuhusu suala la mfumo, Tanzania haina tatizo la kimfumo, kwani iliyopo, iliyowekwa tangu awali na waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume ni imara na imekuwa ikiboreshwa kulingana na mahitaji.


Ifahamike hakuna mahali popote duniani ambako mfumo wa nchi unajiendesha wenyewe, siku zote mfumo huongozwa na kuendeshwa na binadamu ambao kwa udhaifu wa ama kibinadamu au wa kukusudia, hufanya makosa yanayohitaji kusahihishwa kwa taratibu zilizowekwa.

Tatu, Hakuna mtumishi aliyeachishwa au kusimamishwa kazi kwa sababu ya hali ngumu ya uendeshaji wa Shirika lolote, isipokuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji na matumizi mabaya ya ofisi na madaraka, ubadhirifu, uhujumu uchumi na ufisadi.


Chama Cha Mapinduzi kina ushahidi wa utendaji wa Ndugu Lowasa akiwa Waziri Mkuu namna alivyoendesha zoezi la kusimamisha na kufukuza kazi na kuwadhalilisha watumishi bila kufuata taratibu, hali hiyo ni tafauti sana na hii ya sasa, kwani kila anayesimamishwa kazi, anasimamishwa kwa kufuata taratibu zote, ili kuhakikisha kila mtumishi anatendewa haki ya kusikilizwa.


Na katika hili la kuwasimamisha kazi watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wizi na matumizi mabaya ya ofisi, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuunga mkono, kutokana na baadhi yao kuwa kikwazo cha shughuli za maendeleo nchini.


Kiongozi au mwanasiasa anayemkosoa Rais Magufuli katika hatua anazozichukua hivi sasa, ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, ni wa kutiliwa shaka kwani kufanya hivyo ni sawa na kutetea wizi, ufisadi na uporaji wa rasilimali za nchi.


Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
08/04/2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post