JWTZ YATOA TAARIFA KUHUSU TUHUMA YA KASHFA YA NGONO HUKO CONGO




Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kwa taarifa zinazo lituhumu JWTZ kuhusu unyanyasaji wa kijinsia unaodaiwa kufanywa na Wanajeshi wetu kwa Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


JWTZ chini ya Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) limekuwa likitekeleza majukumu ya Ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo takribani miaka mitatu sasa.Katika muda ambao JWTZ limekuwa nchini Congo hapakuwepo na tuhuma kama hizo.


Aidha, JWTZ limetekeleza na limeendelea kutekeleza majukumu kama hayo katika nchi mbalimbali duniani kama vile Msumbiji, Liberia, Visiwa vya Comoro (Anjouan), Lebanon, Sudan katika jimbo la Darfur na sehemu nyingi kama hizo.


Katika kutekeleza majukumu hayo JWTZ limeyatekeleza kwa nidhamu na weledi wa hali ya juu.JWTZ limekuwa moja ya majeshi mengi yanayofanya vizuri na kutoa mchango mkubwa katika Ulinzi wa amani katika nchi ambazo limetekeleza majukumu hayo.


Hivi karibuni kumezuka tuhuma nchini Congo kuhusu Wanajeshi wa JWTZ kuwanyayasa kijinsia wananchi wa Congo.


Kimsingi JWTZ haliwezi kupuuzia taarifa hizo, hivyo limeanza kuchukuwa hatua za kiuchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo ingawa rekodi za majukumu ya ulinzi wa amani zilizokwisha fanywa na JWTZ sehemu mbalimbali zinaonesha kuwa hakukuwa na tuhuma kama hizo.


Kufuatia tuhuma hizo, JWTZ kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa unafanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na ukweli wake. JWTZ halitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika katika tuhuma hizo.


JWTZ bado lipo imara na linaendelea kutekeleza majukumu yake nchini Congo kwa kufuata sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa.


Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Simu: 0784-477638/0756-716085
Email:ulinzimagazine@yahoo.co.uk

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post