SERIKALI imesitisha huduma za tiba asili zitolewazo na Kiliniki za Kikorea, Maibong Sukidar Medical na Korea Medical Clinic zilizopo Jijini Dar es Salaam kwa kosa la kutokuwa na kibali kwa zaidi ya miaka nane pia kuchanganya tiba asili na za kisasa na mbadala bila ya idhini kutoka baraza la usajili la tiba asili nchini
Hatua ya kufungwa kwa kliniki hizo imechukuliwa jana baada ya Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kufanya ziara ya kushtukiza kukagua vibali na huduma zitolewazo katika kiliniki hizo.
Kigwangalla alizitaja sababu zilizopelekea kufungwa kwa Kiliniki ya Korea Medical kuwa ni pamoja na Kutibu magonjwa ambayo haikupewa kibali kutoka serikalini na kuhifadhi dawa ambazo hazihusiani na magonjwa inayotibu
“Kliniki hii ninaamuru ifungwe kwa makosa matano ikiwemo kosa la kuchanganya tiba asili na kisasa, kutokuwa na kibali, usajili halali, matabibu wake hawajui lugha ya Kiswahili na au kiingereza, usajili ulimtaka kuajiri tabibu wa kitanzania ambaye hapa hayupo,” alisema Kigwangalla.
Alisema kliniki hiyo inatumia dawa kali za maumivu, usingizi, uzazi wa mpango, sindano na dripu.
Kigwangala alimwamuru msajili wa hospitali binafsi kufanya uchunguzi ili kubaini hizo dawa zilikuwa zinafanya kazi gani.
Aidha, Kigwangalla alieleza sababu ya kufungwa Kliniki ya Maibong ni pamoja na kutokuwa na kibali kwa zaidi ya miaka minane, kuchanganya tiba asili na kisasa na kutoplekea vyeti vya matabibu wake kama serikali ilivyomtaka kuvipeleka toka mwaka 2008.
“Kiliniki hii haina kibali walichonionesha ni barua walizoandika za kuomba kibali kutoka serikalini na kwamba serikali iliwaambia kupeleka vyeti vya matabibu wake jambo ambalo hawajalifanya hadi sasa,” alisema.
“Baraza la usajili tiba asili lifungie kliniki hadi itakaporekebisha nyaraka zake pamoja na kufanyiwa uchunguzi kama inakidhi vigezo vya kutoa huduma ya tiba asili na mbadala,” amesema.
Kigwangalla alitoa agizo kwa baraza la usajiri la tiba asili nchini kuzifungia kliniki hizo hadi zitakapofuata utaratibu, pia aliitaka idara ya uhamiaji kuchunguza vibali vya makazi na ufanyaji kazi nchini.
Social Plugin