Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Lugumi Akaangwa Bungeni


Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) haijaridhishwa na majibu yaliyotolewa na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi kuhusu Mkataba wa Lugumi Enterprises, na hivyo kamati hiyo imeamua kuunda kamati ndogo leo itakayochunguza kwa undani sakata hilo ambapo ripoti ya uchunguzi huo itawasilishwa bungeni kama ilivyokuwa sakata la Escrow.


Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka chanzo cha kuaminika, PAC haikuridhishwa na majibu ya hoja nyingi zilizotolewa na watendaji wakuu akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu mkataba wa Lugumi baada ya kukutana nao jana mjini Dodoma.


“PAC imelazimika kuunda kamati ndogo kesho (leo), itakayokuwa na nguvu kuhoji mambo yote ukiwemo mkataba huo kwa sababu majibu yaliyotolewa hayakuridhisha,” kilieleza chanzo hicho.


Kiliongeza kuwa baadhi ya mambo yanayokanganya PAC ni kufahamu nani mkweli kati ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia taarifa ya ukaguzi na maelezo ya Jeshi la Polisi kuhusu gharama za mkataba.


Kwa mujibu wa chanzo chetu, taarifa ya CAG inaonesha kuwa mkataba huo ni wa Sh bilioni 37.742 wakati maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Jeshi hilo walipohojiwa na PAC hiyo jana, walisema ni Sh bilioni 37.163.


Hivyo kuwepo kwa tofauti ya zaidi ya Sh milioni 578.972. Aidha, utata mwingine ni jeshi hilo kukosa maelezo ya kwa nini katika kutafuta mzabuni kwenye mradi huo, walitumia mfumo wa mzabuni mmoja badala ya wengi.


Chanzo chetu kilisema katika mahojiano na viongozi hao wa polisi, walishindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kwa nini kitengo cha manunuzi cha jeshi hilo walitumia mfumo huo.


Hivyo kutokana na utata huo, Kamati hiyo imeamua kukutana na Spika leo ili kumtaarifu hatua waliyofikia ya kuunda Kamati Ndogo.


Juzi, taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises ulioshinda zabuni mwaka 2011 ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi vya wilaya nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37, ulitua ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuanza kujadiliwa.


Akizungumza juzi bungeni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo ilifikishwa bungeni Jumatatu na juzi asubuhi wamepewa na wakaanza kuujadili.


Awali, Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam, Kamati hiyo ilitoa siku saba kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga mashine 108 katika vituo tajwa nchini ila hadi sasa ni vituo 14 tu ndivyo vilivyofungwa mashine hizo.


Hatua hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainika kuwa na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.


Ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni pamoja na kampuni hiyo kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye thamani ya Sh bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com