Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Majambazi Watatu Wauawa Katika Jaribio La Uhalifu Wilayani Chunya Mkoani Mbeya


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya (Hawapo pichani)katika kuzungumzia tukio la kuuawa kwa majambazi watatu wakati wakijaribu kufanya uhalifu katika duka la kuuzia vinywaji mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine ambayo ilikuwa ikitumika na majambazi hao katika tukio la kutaka kufanya uhalifu kwenye duka la vinywaji mali ya Hamisi mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya April 27 mwaka huu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha silaha aina ya panga ambalo linadaiwa kutumiwa na majambazi hao .

Baadhi ya askari polisi wakifuatilia kwa makini mkutano wa kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa mbeya Butusyo Mwambelo wakati akizungumza na waandsihi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa majambazi watatu waliotaka kufanya uhalifu katika duka la vinywaji vya jumla linalomilikiwa na ndugu Hamisi Mkazi wa Matundasi Chunya Mkoani Mbeya .

Silaha mbalimbali zilizo kamatwa katika tukio la kuuwawa kwa majambazi wilayani Chnua mkoani mbeya April27 mwaka huu.


JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA.
Mnamo tarehe 27.04.2016 majira ya saa 20:00 usiku huko katika Kijiji na Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliuawa katika majibizano ya risasi na askari polisi wakiwa katika harakati za kufanya uhalifu kwenye duka bia la jumla mali ya bwana HAMIS mkazi wa Matundasi.

Inadaiwa kuwa majambazi hao wapatao watano walikuwa wakitumia pikipiki mbili huku pikipiki moja ikibeba majambazi watatu na nyingine majambazi wawili huku wakiwa na silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine walitaka kufanya uhalifu kwenye duka la jumla la kuuza bia mali ya HAMISI.

Kutokana na taarifa za siri/intelejensia, Jeshi la Polisi lilijipanga kukabiliana na majambazi hao na katika majibizano ya risasi, jambazi mmoja ambaye alikuwa na silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120, risasi 26 kwenye magazine aliuawa baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi tumboni na mguuni na aliweza kufahamika kwa jina moja BARAKA, anayekadiliwa kuwa na umri kati ya 35 hadi 38, fundi ujenzi mkazi wa Makongolosi.

Aidha majambazi wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea kijiji cha Matondo na ndipo askari polisi waliendesha msako mkali kuelekea kijiji hicho na majambazi hao baada ya kuwaona Polisi waliwasha pikipiki zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi ovyo ndipo Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi wengine wawili na kukamata Pikipiki moja yenye namba ya usajili MC 761 AFS aina ya Sanlg iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao.

Majambazi wengine wawili walikimbia na msako mkali unaendelea ili kuwakamata. Miili ya marehemu imehifadhi katika Hospitali ya Wilaya Chunya.

Wito:
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Butusyo A. Mwambelo anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri ili kuzuia vitendo vya kihalifu mapema kabla ya kutokea.

Imesainiwa na:
 [BUTUSYO A. MWAMBELO – SSP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com