Mamlaka Ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Yatoa Tahadhari Ya Kunyesha Mvua Kubwa Wiki Hii




MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa inayozidi milimita 50 wiki hii.


Imesema mvua hizo ambazo zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba zitakuwa kubwa na kuweza kusababisha madhara.


Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi ilisema mvua hizo zilitarajia kunyesha kuanzia Aprili 13, mwaka huu hadi Jumamosi Aprili 16, mwaka huu.


Dk Kijazi alisema kiwango cha uhakika wa mvua hizo ni kwa asilimia 70 na hali hiyo imetokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua sambamba na uwepo wa kimbunga cha Fantala katika Bahari ya Hindi.


Hivyo aliwataka wananchi wanaokaa maeneo yaliyotajwa kuchukua hadhari na kuchukua hatua stahili ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo kubwa.


Hivi karibuni, TMA ilisema mvua za masika katika ukanda wa Pwani zilizoanza wiki ya kwanza ya mwezi huu kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa zitakazoweza kusababisha mafuriko.


Aidha, kwa wakati huo hali ya joto kali itaendelea kuwepo nyakati za usiku huku ikipungua nyakati za mchana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post