Mbunge Wa CHADEMA Amlipua Rais Magufuli, Amtaka Alipe Kodi Kutoka Kwenye Mshahara Wake


Suala la mshahara wa Rais, limeibuka tena bungeni ambapo Bunge limeelezwa kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais hawezi kujipunguzia mshahara pindi anapoapishwa kushika wadhifa huo.


Hayo yalisemwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, kupitia taarifa aliyoitoa kwa Bunge baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema) kumuomba Rais John Magufuli kujipunguzia mshahara.


Mbunge huyo aliyasema hayo wakati akijadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/17 hadi 2021, ambapo pamoja na kusifu jitihada za Rais Magufuli kwa kuonesha dhamira ya wazi ya kuwajali wananchi masikini na kudhibiti matumizi ya serikali, alimuomba kupunguza mshahara wake na pia kuruhusu ukatwe kodi.


“Kwa kweli kwa dhati kabisa nampongeza sana Rais Magufuli kwa namna anavyoonesha wazi kwamba ana dhamira ya kuwatumikia Watanzania. Kwa namna anavyokwenda ni wazi kwamba Rais Magufuli anakuwa Rais wa pili kuwa na mapenzi ya dhati kwa Watanzania baada ya Rais Nyerere (Julius- Baba wa Taifa).


“Pamoja na hayo, kama anataka awe kama Mwalimu Nyerere basi ni wakati sasa wa Rais Magufuli kuchukua hatua za kujipunguzia mshahara wake na pia kuruhusu mshahara wake kukatwa kodi, hili litampa heshima kubwa sana Rais wetu,” alisema Peneza.


Akitoa taarifa kwa Bunge, Waziri Simbachawene alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake, Ibara ya 43, Ibara ndogo ya 3, Ukurasa wa 62 inamzuia Rais kupunguza mshahara akiwa madarakani.


Alisema; “Ibara hiyo inasema hivi: ‘Mshahara na malipo ya Rais, havitapunguzwa wakati Rais anapokuwa bado anashika madaraka yake.


“Rais aliyepo sasa hawezi kujipunguzia mshahara wake yeye mwenyewe isipokuwa anapoondoka anaweza kuweka kiwango cha mshahara cha Rais ajaye.


"Kwa hiyo wakati wabunge mnaendelea kumuomba Rais apunguze mshahara wake ni lazima mjue jambo hilo ni kinyume cha Katiba”.


Ufafanuzi huo wa Waziri umekuja siku chache wakati Rais Magufuli akiwa tayari amejitangazia mbele ya umma kiwango cha mshahara anacholipwa akisema ni Sh milioni 9.5 kwa mwezi.


Rais aliyasema hayo akiwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita wakati alipokwenda kwa mapumziko mafupi hivi karibuni, hatua ambayo ilipokelewa kwa shangwe na wananchi wengi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post