Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christina Mughwai Lissu amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani leo.
Kaka
wa marehemu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
alituma taarifa kwenye mitandao ya jamii akisema amepata taarifa za
msiba huo akiwa mkoani Kigoma.
Alisema Christina alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam na alianza kuugua tangu mwaka jana.
“Nawasalimu
kutoka Kibondo. Nina habari zisizokuwa njema. Dada yangu aliyekuwa
mbunge wetu wa viti maalumu, Christina amefariki dunia muda mfupi
uliopita katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
“Marehemu
alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ‘cancer’ tangu mwaka jana. Kwa sasa
niko nje ya Dar es Salaam na ndiyo kwanza taarifa hizi zimenifikia…” ilisema taarifa ya Lissu aliyoituma mitandaoni.
Christina
alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Singida tangu mwaka 2010 hadi
2015 na alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha. Hakurudi
bungeni katika uchaguzi wa 2015.