MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amewaomba wananchi wa wilaya ya Ruangwa kuwaombea dua viongozi wa taifa, Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili waweze kufanya kazi zao kikamilifu.
Amesema kazi nzito inayofanywa na viongozi hao ya kuhakikisha nchi inakuwa salama na inasonga mbele kimaendeleo ni shughuli ngumu na inahitaji nguvu ya Mungu, hivyo ni vema wananchi wakawaombea dua ili kazi hiyo iweze kuwa na tija kwao na taifa kwa ujumla.
Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Chinongwe wilayani Ruangwa, ambapo amewaomba mwananchi hao wajitahidi kuwaombea dua viongozi hao ili malengo yao ya kuwaletea maendeleo yatimie.
Mary ameongozana na Waziri Mkuu Majaliwa ambaye ni mbunge wa Ruangwa, katika ziara yake ya kuwashukuru wananchi waliomchagua kwa nafasi ya ubunge na kisha Rais Dk Magufuli kumteua kuwa kushika wadhifa huo.
"Nawashukuru sana wananchi kwa kuwa kura zenu ndiyo zilizosababisha Mheshimiwa Majaliwa ambaye ni mbunge wetu kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, hivyo nawaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana,” amesema mke wa Waziri Mkuu.
Amesema licha ya kuongezewa majukumu atahakikisha anaendelea kushirikiana na wanaruangwa ili waweze kuendeleza shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo na kwamba wasiwe na wasiwasi kwani hata wasahau kwa kuwa anawapenda na kuwaheshimu.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.