Mwanafunzi wa kidato cha tatu, juzi alimkaanga askari polisi anayedaiwa kumbaka kwa kuieleza Mahakama jinsi alivyotendewa kitendo hicho katika kibanda cha ulinzi cha benki.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Misungwi,mkoani Mwanza Ruth Mkisi, shahidi huyo alidai siku ya tukio askari huyo, Raphael Sixstus (30), alimuita alipokuwa akipita karibu na Benki ya CRDB Tawi la Misungwi, alipoitikia wito ghafla alivutiwa ndani ya kibanda hicho na kumbaka.
“Wakati akinitendea kitendo hicho, alikuwa akinitishia kisu huku akiniambia nikipiga kelele ataniua, niliogopa nikaa kimya ingawa niliumia na kutokwa damu nyingi sana,” alidai shahidi huyo.
Akiongozwa na Mwendasha Mashtaka wa Polisi, Doreth Mgenyi, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16 alidai kabla ya kumbaka, mshtakiwa huyo alimvua nguo zote za ndani.
Awali, Mwendesha mashtaka alipokuwa akimsomea makosa mshtakiwa huyo alidai kuwa Novemba 20, mwaka jana, akiwa eneo la lindo katika Benki ya CRBD Tawi la Misungwi, alimbaka mwanafunzi huyo saa 1.00 usiku wakati akitoka mashine kusaga unga katika maeneo ya Bomani.
Hakimu Mkisi aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kuita mashahidi wengine. Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana.
Social Plugin