Msemaji Mkuu wa CCM ambaye pia ni Mjumbe wa NEC, Christopher Ole Sendeka akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kata ya Bashneti, wilayani Babati mkoani Manyara alisema, Chama Cha Mapinduzi kinamuunga mkono na kumtetea kwa nguvu zake zote Rais Dk. John Magufuli katika jitihada zake za kuliinua taifa la Tanzania.
Alisema, CCM itafanya hivyo kwa sababu kazi anayoifanya ya kupambana na wazembe na wezi wa mapato kwenye vyanzo vya uchumi wa taifa inatokana na maelekezo ya ilani ya CCM.
Sendeka alisema, CCM inawataka wale wote wanaojaribu kupotosha jitihada zinazofanywa na Rais za ‘kupasua majipu’ wakidai kuwa ni kuwaonea wanaochukuliwa hatia, kuacha mara moja, kwa sababu kinachofanyika ni sahihi na kipo kwa mujibu wa sheria.
Alisema, upasuaji majipu huo unaofanaywa na Rais Magufuli hauchagui chama bali yeyote anayebainika kuwa ni jipu hata akiwa mwana CCM haachwi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa NEC, Kilumbe Ng’enda, aliwataka Watazania kutambua kuwa Uchaguzi umeshamalizika kwa hivyo asitokee yeyote kuanza kuweweseka, kwa kutoa maneno ya kejeli kuhusu utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli kwa sababu baada ya uchaguzi kumalizika sasa kiichobaki ni kuchapa kazi.
Alisema, hakuna sababu za mwanasiasa yeyote kuanza mambo ya fitina za kisiasa wakati huu kwa kuwa kufanya hivyo ni kujisumbua.