Kamati ya kudumu ya Bunge inayoshughulikia Hesabu za Serikali (PAC) imeunda kamati ndogo ya watu tisa itakayochunguza kwa kina mkataba uliozua utata wa Sh37bilioni ulioingiwa baina ya Jeshi la Polisi na Lugumi Enterprises.
Pande hizo mbili, Jeshi la Polisi na Lugumi Enterprises, ziliingia mkataba huo kwa ajili ya kufunga vifaa 108 vya kuhifadhia alama za vidole katika vituo vya polisi.
Akizungumza na wanahabari leo mjini Dodoma, makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilary amesema kamati hiyo itafanya kazi kwa siku 30, kuanzia Jumatatu ijayo.
Wajumbe tisa wa kamati hiyo ndogo ni; Japhet Hasunga (Vwawa-CCM), wengine wa CCM ni Livingstone Lusinde (Mtera), Stanslaus Mabula (Nyamagana), Haji Mponda (Malinyi) na Hafidh Ali Tahir (Dimani).
Wabunge wa upinzani waliopo katika kamati hiyo ni Nahenjwa Kaboyoka (Same Mashariki-Chadema), Musa Mbaruk (Tanga Mjini-CUF), Tuza Malapo (Viti Maalum-Chadema) na Khadija Nassor Ali (Viti Maalum-CUF).
Social Plugin