Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Rais Magufuli Amtumbua Jipu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Wilson Kabwe Darajani



Rais Magufuli amemsimamisha kazi leo mchana  Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Wilson Kabwe kutokana na ufisadi wa kutisha katika utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji magari katikati ya mji na kuisababishia serikali hasara ya bilioni 3. 





Rais Magufuli amechukua uamuzi huo leo mchana  wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni, ambapo kabla ya Rais kuhutubia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitoa Hotuba fupi ya maswala kadhaa ya Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo ripoti ya tume aliyounda kuchunguza utekelezwaji wa mikataba hiyo. 




Akieleza zaidi, Makonda amesema, Kamati aliyounda ilibaini kuwa pale ubungo kunatumika sheria ndogo mbili za ukusanyaji mapato moja ya mwaka 2004 na nyingine ya mwaka 2009 ambazo zote zilisainiwa na Wilson Kabwe. 




Amesema kuwa Sheria ya Mwaka 2004 ya ukusanyaji mapato, inaonesha kuwa kila basi linaloingia Ubungo linatakiwa kutozwa Sh 4,000, hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na mabasi 350 yanayoegeshwa kituoni hapo na Sheria ya Mwaka 2009 ya ukusanyaji mapato, inaonesha kuwa kila basi linaloingia Ubungo linatakiwa kutozwa Sh 8,000, hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 82 kwa mwezi.




Makonda amesema kwamba, Kabwe alisaini mikataba miwili, wa 2004 na wa mwaka 2009 ambapo ule wa mwakla 2004 ulipelekwa jiji na ule wa 2009 ukapelekwa kwa mzabuni, hivyo jiji wanajua kuwa basi linatozwa sh. 4000 kwa mwezi wakati mzabuni anatozwa 8000 kwa mwezi. 




Kutokana na maelezo hayo, Mheshimiwa Rais ametangaza kumsimamisha kazi bwana Kabwe ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na ameagiza vyombo vya dola vianze uchunguzi mara moja ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com