Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Spika Apangua tena Kamati za Bunge, Wabunge Wapinga Wadai Linapunguza Ufanisi


Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko mengine ya kamati za Bunge kwa kuwaongeza wabunge wapya na kuwahamisha wengine kwenda kwenye kamati nyingine, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wabunge wakidai linapunguza ufanisi.


Juzi, Spika Ndugai (pichani) aliwaongeza wabunge wanne wapya walioapishwa bungeni Aprili 19, kwenye kamati za Miundombinu; Ardhi, Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Maji; na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.


Hayo ni mabadiliko ya pili tangu Bunge la 11 lianze rasmi vikao vyake katikati ya Novemba mwaka jana, ikiwa ni kipindi kifupi cha mabadiliko ikilinganishwa na Bunge la Tisa na 10.


Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Bunge, mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2016, ili kuhakikisha kila mbunge anakuwa mjumbe wa kamati mojawapo ya Bunge.


“Aidha, mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kadri itakavyowezekana, Muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge unazingatia aina za wabunge kwa jinsia, pande za Muungano na Vyama vya Siasa vyenye uwakilishi bungeni, ujuzi maalumu, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na matakwa ya wabunge wenyewe,” inasema taarifa hiyo.


Baadhi ya wabunge jana walipinga mabadiliko ya mara kwa mara ya wajumbe wa kamati, wakieleza kuwa hayaleti tija na uamuzi huo haufanywi kwa umakini.


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema mabadiliko hayo yanaonyesha namna ambavyo Spika Ndugai “anavyokosa umakini katika uundaji wa kamati hizo”.


“Spika hakuwa makini wakati anaziunda kamati hizo na sina jingine zaidi ya kusema, maana hilo liko wazi,” alisema Zitto.


Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema uundaji wa kamati kila mara, unatokana na kiongozi huyo kutokuwa na umakini na mara nyingi anafanya kazi kwa shinikizo la vikao vya chama.


Msabaha alisema utaratibu wa kuvunja kamati na kuziunda unatokana na vikao vya wabunge wa CCM, ambavyo humshauri Spika juu ya nini kifanyike ili waweze kuubana upinzani, ushauri ambao anadai wakati mwingine unakosa tija.


Mbunge wa Sengerema William Ngeleja (CCM) alisema mabadiliko yanayofanywa hayana madhara yoyote, kwa kuwa ni jambo la kawaida kufanya maboresho na kuwataka wabunge kujifunza kupitia mchezo wa mpira ambao kila mtu anakuwa na namba yake, lakini uwanjani anacheza namba zote.


“Waangalie mfano wa Profesa Makame Mbarawa ambaye alipewa Wizara ya Maji, lakini akaondolewa baada ya wiki tatu na kupelekwa kusimamia barabara ambako ameonyesha uwezo mkubwa, iweje kwa wabunge?” alihoji Ngeleja.


Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema mabadiliko yanayofanywa hayawezi kuleta tija katika bunge hilo, kwani watu wanashindwa kujipanga vyema kwa kuwa hawajui kesho itakuwaje.


Lugola alihoji juu ya mafunzo waliyopata kila kamati, lakini wanabadilishwa bila utaratibu huku akisema hata kamati ya uongozi inaathirika zaidi, kwani wanapobadilishwa na kuondolewa wenyeviti lazima kamati ya uongozi ibadilike.


Spika Ndugai hakupatikana jana kueleza kwa kina mabadiliko hayo. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema siyo msemaji na Ndugai na ndiye angepaswa kuulizwa jambo hilo.


Katika taarifa hiyo ya Bunge, Spika Ndugai aliwataka wajumbe wa kamati sita ambazo hazina viongozi kuwachagua mapema iwezekanavyo kama kanuni za Bunge zinavyohitaji.


Kamati hizo ni Hesabu za Serikali (PAC) Mwenyekiti; Kamati ya Nishati na Madini, (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Mwenyekiti) na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Makamu Mwenyekiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com