Kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa baadhi ya wafanyabiashara wameficha sukari ili kutengeneza uhaba sokoni utakaopandisha bei ya bidhaa hiyo, imedhihirika baada ya baadhi ya wafanyabiashara hao kuanza kukamatwa wakiwa na vidhibiti.
Kutokana na hali hiyo iliyosababisha bei ya bidhaa hiyo kuanza kupanda, Waziri Mkuu Majaliwa, alitangaza uamuzi wa Serikali kuagiza sukari yake nje itakayouzwa kwa bei elekezi kwa wananchi ya Sh 1,800 kwa kilo, ili kuzuia ongezeko hilo haramu la bei.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi alitangaza polisi kuwashikilia wafanyabiashara wawili wa mjini hapa kwa tuhuma za kukutwa na zaidi ya mifuko 655 ya sukari, sawa na tani 24.3, ikiwa imekifichwa kwenye stoo zao.
Kwa mujibu wa Amanzi, wafanyabiashara hao walikamatwa kwenye msako ulioendeshwa na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa Singida pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Amanzi alisema kuwa msako huo uliendeshwa baada ya kupata taarifa za siri kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wameficha sukari, ili waje kuiuza kwa bei ya juu kwa wateja wao kwa kisingizio kuwa kuna uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo.
“Katika msako huo, tumemnasa Mohamed Alute Ally (44), mfanyabiashara wa eneo la Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39), mfanyabiashara wa eneo la Minga katika manispaa ya Singida aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa mwito kwa wafanyabiashara wote kuacha kuficha bidhaa zote muhimu, ikiwemo sukari na mchele, bali waiuze kwa bei halali kwa wateja wao.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Mchina, amesema msako mkali unaohusisha kikosi kazi maalumu pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama utaendelea kwa nguvu zote na kusisitiza kuwa kuhodhi bidhaa kwa sababu yoyote ile ni kosa la uhujumu uchumi.
Mmoja wa Wakala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi Mjini, Salim Nagji, amesema mfuko mmoja wa sukari huuzwa Sh 92,650 lakini tangu sukari iadimike mfuko unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na Sh 2,800 kwa kilo kinyume na bei elekezi ya Sh 1,800.