Wakuu wa wilaya za Kinondoni na Musoma wameapishwa leo baada ya kuteuliwa mapema wiki hii na Rais John Magufuli.
Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amemwapisha mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Salum Hapi, aliyeteuliwa Aprili 18.
Ali Hapi amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Makonda ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mwezi uliopita.
RC Makonda amempa DC huyo vipaumbele saba vya wilaya hiyo, ambavyo alisema kuwa ni pamoja na afya, haki ardhi, rushwa, kero na kushughulikia migogoro.
"Natuma salamu kwa wala rushwa na mafisadi wote waliopo Wilaya ya Kinondoni, wanaopora haki za wananchi na rasilimali za nchi ili kujinufaisha wao na familia zao. Nitapambana nao usiku na mchana kuhakikisha ninashinda vita hii," alisema Ali Salum Hapi.
Naye mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo amemwapisha Humphrey Polepole kuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma baada ya kuteuliwa Aprili 18 kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Zelothe Stephen aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa.