Dawa inayotumika kwa matibabu ya kawaida huenda ikategua kitendawili cha kurefusha maisha na kuzuia uzee.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya, ambao ulibainisha kwamba viwango vya chini vya dawa aina ya Lithium vilisaidia kurefusha maisha ya nzi waliowekwa kwenye maabara.
Wanasayansi wamesema utafiti huu unatoa matumaini ya kutoa dawa kuwasaidia watu kuishi maisha marefu na yenye afya.
Lithium inatumika katika matibabu ya matatizo ya akili, kama mfadhaiko, na kusongwa na mawazo.
Hata hivyo ina madhara makubwa ikiwa itatumika kwa viwango vya juu.
Haijulikani jinsi Lithium inavyotibu matatizo ya akili, lakini alipopewanzi, dawa hiyo ilisaidia kurefusha maisha yao.
Hata hivyo watafiti wamesisitiza lazima dawa hii kutumiwa kwa viwango vya chini zaidi, kwani viwango vya juu vinaweza kuleta maafa.
Dkt Ivana Bjedov mmoja wa watafiti kutoka taasisi ya matibabu ya saratani amesema dawa hii itasaidia afya kwa wazee sawa na kuzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa kutetemeka 'Parkinson'.
Kando na matatizo ya akili Lithium imetumika kutibu maumivu makali ya kichwa 'Migraines' na ugonjwa wa jongo unaomfanya mtu kuvimba viungo hasa wakati wa baridi.