Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametishia kufuta halmashauri zitakazoshindwa kukusanya mapato kufikia asilimia 80 ya lengo na kuwaonya watumishi wa halmashauri hizo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya kodi na tozo mbalimbali, kutozipa kampuni zao kazi hiyo kuepuka mgongano wa kimaslahi.
Majaliwa alisema endapo mtumishi wa halmashauri atabainika kutumia kampuni yake kukusanya kodi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema hayo jana mjini Dodoma, wakati akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT).
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika uboreshaji wa huduma za wananchi na ukusanyaji mapato, hivyo halmashauri itakayoshindwa kukusanya mapato kwa asilimia 80 itafutwa.
Alisema kumekuwa na ufujaji mkubwa wa mapato kupitia mawakala na watumishi wachache wasio waaminifu. Alitaka mapato yote ya halmashauri yakusanywe na kusimamiwa vizuri kwa njia za kielektroniki kwa kuwa ndio njia salama.
“Njia za kielektroniki ni salama na itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mapato,” alisema.
Alisema, mkakati wa kuwezesha halmashauri kuwa na miradi na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato lazima uheshimiwe hasa wakati huu ambao Serikali inasisitiza umuhimu wa kujitegemea yenyewe.
“Niwakumbushe watendaji wote, tukibaini taarifa za watumishi wa halmashauri kumiliki kampuni za kukusanya ushuru na tozo mbalimbali, hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Ni dhahiri kuwa huko ni kuleta mgongano wa kimaslahi,” alisema.
Aliongeza kuwa, rushwa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi katika maeneo yote hususan kwenye huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali katika Serikali za Mitaa.
“Wananchi wanakosa haki zao na maisha yao yanaendelea kuwa duni kutokana na hali iliyojitokeza ya dhuluma, ufisadi na jeuri wanayofanyiwa na watoaji na wapokeaji wa rushwa. Rushwa ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ya halmashauri, Serikali Kuu na taasisi mbalimbali za umma,” alisema Majaliwa.
Aliwataka viongozi wa halmashauri kuikomesha kwa kuwa inalalamikiwa kwenye maeneo yao na kuondoa ubadhirifu katika ukusanyaji wa mapato, matumizi mabaya ya madaraka na kukomesha utekelezaji wa miradi chini ya viwango.
Aliwataka viongozi wakuu kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha hakuna huduma inayotolewa kwa kutoa rushwa. Pia, alisema Serikali itaendelea kuimarisha misingi ya kikatiba na namna ya mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali Kuu na za mitaa, lengo likiwa kuhakikisha mipango wanayosimamia inaleta manufaa kwenye maeneo yao.
“Wakuu wa mikoa na wilaya wana uwezo wa kuhoji chochote hakuna zuio, lakini hatujaruhusu Mkuu wa Wilaya kuomba fedha, anatakiwa akague miradi na ajiridhishe kuwa inatekelezwa ipasanyo kwa thamani ya fedha inayotengwa,” alisema.
Alisema, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya hahitaji posho kwenye vikao vya halmashauri hivyo wasiogope kuwaalika kwenye vikao vyao. Akizungumzia migogoro ya ardhi, Majaliwa alisema, imekuwa mingi hali inayotoa somo kuwa sasa Watanzania wanajua thamani ya ardhi.
Alisema ili kuondoa migogoro iliyopo, lazima kila halmashauri iwe na mipango ya matumizi bora ya ardhi kuanzia vitongojini mpaka vijijini. Alitaka wananchi waitambue mipaka yao kwa sababu hiyo si kazi ya Waziri bali ni ya halmashauri yenyewe na kila kijiji.