Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka makatibu tawala wa mikoa nchini kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliosababisha kuwapo kwa watumishi hewa.
Amesema suala hilo la watumishi hewa limeisababishia Serikali hasara kubwa, hivyo ni lazima watu wote waliohusika katika sakata hilo wabainishwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Lindi iliyowasilishwa na mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi katika siku ya kwanza ya ziara yake ya pili kikazi wilayani Ruangwa.
Wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa Machi 15, Rais John Magufuli aliwapa siku 15 kuhakikisha wanabaini watumishi hewa wote katika mikoa yao na kuwaondoa katika mfumo wa malipo.
Baada ya kufanyika kwa kazi hiyo, jumla ya watumishi hewa 7,795 walibainika ambao wameisababishia Serikali hasara ya Sh7.5 bilioni.
Awali, Zambi alisema Lindi ina jumla ya wafanyakazi watoro 57 na hewa saba ambao walifariki na wengine kustaafu, lakini walikuwa wakilipwa mishahara na kuisababishia Serikali hasara ya Sh36 milioni kwa mwezi.