Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka Rais John Magufuli kukabiliana na vikundi vya mafisadi vinavyoiba mabilioni ya fedha za umma kupitia mikataba mibovu waliyoingia badala ya kuishia kutumbua majipu.
Akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake jana, Zitto alisema ACT Wazalendo inaunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kupambana na ufisadi, lakini bado hajagusa kiini chenyewe.
Zitto alitolea mfano wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa bado kuna kampuni inayolipwa Sh8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya mitambo yake ya umeme.
Pia, alisema kashfa ya hati fungani imeongeza deni la Taifa kwa Sh1.2 trilioni.
“Bado huo mtambo upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa Sh8 bilioni wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndivyo vikundi masilahi katika sekta ya nishati. Bila kuvibomoa, Rais ataonekana anachagua watu katika vita hii,” alisema Zitto.
Alisema: “Ni kweli kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa rushwa ya Dola 6 milioni za Marekani zinazohusu hati fungani.
"Serikali imewafikisha mahakamani madalali wa rushwa lakini waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani. Waliopokea rushwa ambao ni maofisa wa Wizara ya Fedha hawajashtakiwa.”
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alisema vita ya ufisadi siyo ya kutumbua majipu tu, bali kujenga mfumo madhubuti wa kuzuia mianya ya rushwa.
Alisema Rais Magufuli anapaswa kuwaongoza Watanzania katika vita ya kukataa mikopo kama hiyo ambayo inawasababishia umaskini.
Aungana na hoja za upinzani
Zitto alisema chama chake kinaungana na vyama vingine vya upinzani kwa hoja walizozitoa baada ya kutoka bungeni za kutokuonyeshwa moja kwa moja kwa matangazo ya televisheni kutoka bungeni, matumizi ya Serikali nje ya mpango wa bajeti na Serikali kutokuwa na mwongozo kwa mawaziri wake.
Akizungumzia kusitishwa kwa urushaji wa matangazo ya Bunge, Zitto alisema hatua hiyo inatakiwa kupigwa vita kwa sababu inajenga udikteta katika nchi na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari za Bunge.
“Ina maana TV zinapaswa kumuonyesha mtu mmoja tu akihutubia bungeni ambaye ni Rais tu... hapana hii siyo sawa,” alisema Zitto.
Akizungumzia suala la bajeti, Zitto alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka Rais kuhamisha fedha kwenda kufanya shughuli nyingine. Lakini alisema tangu Rais Magufuli achaguliwe, amekuwa akihamisha fedha wakati Bunge lilishapitisha bajeti.
“Rais Magufuli kwani amekuwa waziri wa fedha, waziri wa ujenzi na Rais kwa wakati mmoja? Tunamtaka asiingilie majukumu ya mihimili mingine, wananchi tumnyooshee kidole na kumwambia afuate utaratibu,” alisema Zitto.
Mbunge huyo pekee wa chama hicho, alisema tangu walipoapishwa, mawaziri hawajapewa mwongozo wa kazi na kutoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa miongozo kwa mawaziri.
“Mpaka sasa nchi haina mawaziri kwa sababu hawajapewa miongozo. Kwa hiyo, Baraza la Mawaziri lina mawaziri wawili tu ambao ni Rais na makamu wake,” alisema Zitto na kulitaka Bunge kutengeneza mfumo wa kuisukuma Serikali kutekeleza mambo muhimu kwa Taifa.
Kuhusu hali ya uchumi, Zitto alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka mpaka kufikia Sh29 trilioni lakini ana wasiwasi itakwama kwa sababu theluthi moja ya mapato ya ndani yanatoka bandarini ambako ripoti zinaonyesha kuwa yamepungua.
Alisema Serikali imepanga kukopa Sh7 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti na kwamba hatua hiyo inazidi kuongeza deni la Taifa ambalo limelalamikiwa pia na Mkaguzi na Mdhibiti wa Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake.
Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira aliwataka wajumbe wa chama hicho kusimama pamoja ili kukijenga chama hicho na kukifanya kiwe mbadala kwa Watanzania akisema kimewavutia watu wengi ambao wanachukizwa na ufisadi.