Angalia Picha 50!! Mkutano Mkuu Wa Mwaka wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga


Hapa ni katika Msikiti wa Masjid Latif Ahmadiyya Muslim Jamaat Nsalala uliopo kijiji cha Nsalala ,kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga ambapo leo Jumapili Mei 22,2016 Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga (Ahmadiyya Muslim Jamaat Shinyanga) imefanya mkutano wa Mwaka wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Shinyanga ukiwa na kauli mbiu ya " Love For All Hatred For None (Mapenzi Kwa Wote Bila Chuki Kwa Yeyote".

Mgeni rasmi alikuwa katibu tawala msaidizi idara ya  uchumi na uzalishaji mkoa wa Shinyanga Mohammed Idd Nchira aliyemwakilisha kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga John Mongella huku waumini wa dini hiyo kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga wakihudhuria mkutano huo.

Mkutano huo uliolenga kuhamasisha amani katika jamii kwa kuwakumbusha waumini kumjua mwenyezi mungu hali itakayosaidia kupunguza hata kumaliza kabisa vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji ya watu wasio na hatia kama vile vikongwe na albino, umehudhuriwa pia na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry (pichani juu).

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry alieleza kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya watu watu msikitini na kuongeza kuwa dini ya kiislam hairuhusu vitendo kama hivyo huku akiviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kubaini wahusika wa kitendo hicho haramu.

Kupitia mkutano huo jamii imeelimishwa juu ya dhana potofu dhidi ya uislamu ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha dini hiyo pamoja na vikundi vya kigaidi mfano wa Boko haram, Isis, Al-shabaab na vingine vingi ambavyo vimekuwa vikidhuru binadamu. 

Mada mbalimbali zimetolewa na viongozi wa jumuiya hiyo ikiwemo nafasi ya dini katika maisha ya binadamu,malezi ya watoto na majukumu ya wazazi sawa na mafundisho ya dini ya kiislamu,umuhimu wa kuwa kiongozi (Khalifa) wa kiroho na barakaza ukhalifa pamoja na masharti ya kujiunga na jumuiya hiyo(masharti 10 ya Baiat na wajibu wa waumini.

Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde alikuwepo wakati wa mkutano huo,ametusogezea picha 55 kilichojiri..
Hapa ndipo Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga waumini wa dini ya kiislamu kutoka Jumuiya hiyo kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi kusikiliza mawaidha mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na wageni waalikwa akiwemo kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mohammed Idd Nchira
Bango likionesha kilichokuwa kinaendelea 
Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame akitoa mada kuhusu Haja ya nafasi ya dini katika maisha ya binadamu ambapo alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kutenda mambo mema na kujiepusha na vitendo vya kihalifu ikiwemo kuua watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe.

Alisisitiza kuwa uislamu ni dini ya amani hivyo kuwataka binadamu kuishi kwa amani na kwamba kitendo cha kuua mtu mmoja ni sawa na kuua dunia nzima.Hata Hivyo Ame alisema sera ya jumuiya hiyo ni kutochanganya siasa na dini 


Meza kuu,wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry,kushoto kwake ni mgeni rasmi Mohammed Idd Nchira,akifuatiwa na rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa Salim Thani,wa kwanza kushoto ni Naibu rais wa jumuiya hiyo Kanda ya ziwa Yahaya Kamba Ulaya.Wa kwanza kulia ni Mbashiri wa kanda ya ziwa  wa jumuiya hiyo Sheikh Waseem Khan 
Waumini wa dini ya Kiislam kutoka maeneo ya mjini na Vijijini ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga waliojitokeza katika mkutano huo
Mgeni rasmi katika mkutano huo Mohammed Idd Nchira akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Moja ya mabango yaliyokuwa katika mkutano huo
Mgeni rasmi katika mkutano huo Mohammed Idd Nchira akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya ambapo alisema suala amani katika jamii ni watu wote hivyo kuwataka watanzania kudumisha amani ya nchi kwa kuepuka kutenda uhalifu
Aliyesimama ni Afisa wa polisi kutoka ofisi ya mkuu wa upepelezi na makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga Issa Ramadhan akitoa neno ambapo alisema jamii yenye malezi mema haiwezi kuwa na vitendo vya kihalifu na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kuwafichua watu wote wanaofanya vitendo vya uhalifu
Wanawake wa Kiislam wakiwa katika Msikiti wa Masjid Latif Ahmadiyya Muslim Jamaat Nsalala uliopo kijiji cha Nsalala ,kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo wa mwaka,ambapo kwa mara ya pili sasa mkutano kama huo unafanyika mkoani Shinyanga,mkutano mwingine ulifanyika mwaka 2014
Wanawake wakiwa msikitini
Mkuu wa kituo cha polisi Tinde Mkaguzi Msaidizi wa polisi Wilbert Sichone aliyemwakilisha mkuu wa polisi wilaya ya Shinyanga,akitoa neno katika mkutano huo ambapo aliwaomba viongozi wa dini mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya dini kwani vitendo vingi vya kihalifu vimekuwa vikijitokeza kutokana na jamii kutokuwa na hofu
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsalala kilichopo katika kata ya Tinde Sandeko Machongo akitoa shukrani kwa jumuiya hiyo kwa kushirikiana na wananchiwa kijiji hicho katika masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa visima vitatu vya maji
Waumini wakifutilia kilichokuwa kinaendelea kwenye mkutano huo
Mbashiri/Sheikh wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt akitoa mada ya Masharti kumi ya Baiat na wajibu wa waumini wa jumuiya hiyo.Miongoni mwa masharti hayo ni pamojana waumini kutojihusha na vitendo vya kishirikina akieleza kuwa ushirikina ndiyo chachu ya maovu/mabaya yote katika jamii
Tunamsikiliza Mbashiri wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt
Mbashiri wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt alitumia fursa hiyo kuwataka wanadamu kuwapuuza baadhi ya watu wanaodai kuwa jumuiya hiyo haifuati misingi ya dini ya kiislam huku akiongeza kuwa tofauti yao na wengine wao wanafanya misingi ya dini kwa vitendo badala ya maneno
Meza kuu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Tunafuatilia kinachoendelea hapa......
Waumini wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Watoto wakiwa msikitini wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akitoa hotuba yake ambapo pamoja na mambo mengine alisema jumuiya hiyo ambayo ipo katika nchi 207 duniani kila siku imekuwa ikiwakumbusha waumini kuishi katika misingi ya kumfuata mwenyezi mungu,kwasisitiza waumini kushika mafundisho kwa vitendo badala ya maneno ili wawe raia wema ili jamii iishi kwa amani
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry alieleza kusikitishwa na mauaji ya watu watatu jijini Mwanza katika msikiti na kusema kuwa dini ya kiislamu hairuhusu watu kuuana na kuwaomba wakazi wa Mwanza na nchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya uchunguzi ili kujua chanzo cha mauaji na kuwabaini wahusika wa mauaji hao
Mkutano unaendelea
Mkutano unaendelea

Tunamsikiliza Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akisisitiza kuwa jumuiya hiyo ya kimataifa ina uongozi wake na inaendeshwa kwa heshima kubwa na siku zote wamekuwa wakihubiri amani
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akiwaomba watanzania kuachana na vitendo vya kihalifu ikiwemo kuua albino na vikongwe kwa imani za kishirikina
Kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame akitafsiri hotuba ya Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry aliyokuwa anaitoa kwa lugha ya Kiingereza
Kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame akitafsiri hotuba ya Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry aliyokuwa anaitoa kwa lugha ya Kiingereza.Chaudhry alisema ili jamii iishi kwa amani ni vyema binadamu wakaishi kwa kupendana na kuacha vitendo vya kishirikina na kulipishana visasi
Mabango yakiwa katika eneo la mkutano
Mabango yakiwa na ujumbe wa aina mbalimbali katika eneo la mkutano
Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya ina kiongozi mkuu duniani ambaye sasa anaitwa Khalifatul Masih v Hazrat Mirza Masroor Ahmad ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kujitahidi kuwaomba wanadamu kuishi kwa kuzingatia misingi ya amani.
Viongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya wakijiandaa kuomba dua wakati wa mkutano,kushoto ni Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry katikati ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania,kulia ni rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa Salim Thani
Kulia ni rais wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Kanda ya Ziwa Salim Thani akiteta jambo na kiongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza (kushoto)
Kulia ni rais wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Kanda ya Ziwa Salim Thani akiteta jambo na kiongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza (kushoto)
Waumini wa Jumuiya hiyo wakiwa wamesimama wakati wa kuomba dua
Waumini wakiwa tayari kuomba dua
Waumini wakiwa wamesimama wakati wa kuomba dua
Tunaomba dua
Akina mama wakiwa ndani ya msikiti wakiomba dua
Viongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya wakiomba dua wakati wa mkutano,kushoto ni Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry katikati ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania,kulia ni rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa Salim Thani
Kushoto ni Yusuph Mgeleka kutoka mkoa wa Shinyanga ,Mubarak Nyamihasi kutoka mkoani Mwanza(katikati) na Mussa Kaswezi kutoka mkoa wa Kagera(kulia) wakiimba shairi la kuagana wakati wa kufunga mkutano huo
Wanawake na watoto wakiwa nje ya msikiti baada ya mkutano kufungwa
Bango katika mkutano huo
Picha ya kumbukumbu baada ya mkutano huo kumalizika
Bango likiwa katika mkutano huo
Bango likiwa katika mkutano huo wa mkoa wa Shinyanga ulioandaliwa na Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga
Bango likionesha ujumbe mzuri
Bango jingine lilokuwa katika mkutano huo
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog


hotuba ya mheshimiwa mkuu wa mkoa wa shinyanga
Katika mkutano wa mwaka wa jumuiya ya waislamu waahmadiyya kanda ya mwanza, shinyanga na simiyu
tarehe 22 mei 2016

Mheshimiwa Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya
Tanzania,
Sheikh Tahir Mahmood,

Viongozi wa Kamati kuu ya Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya nchini

Viongozi waalikwa wa ngazi mbalimbali

Mabibi na Mabwana;

Assalaam Alaikum, (Amani iwe juu yenu).

Awali ya yote, natoa shukurani zangu za dhati kwa kunikaribisha katika mkutano huu wa Jumuiya yenu ya Ahmadiyya hapa katika Kanda ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu.  

Nimefahamishwa  kuwa wageni mbalimbali kutoka mikoa ya kanda hii wakiwemo viongozi wa kijamii na kisiasa wamealikwa katika mkutano huu.

Mheshimiwa Amir,
Nimefahamishwa pia kwamba Jumuiya yenu ya Ahmadiyya imekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 80 sasa na kwamba katika muda huo wote imeonyesha mfano mzuri wa upendo na kuvumiliana na waumini wa itikadi zingine hapa nchini. Hali hiyo ni licha ya kuwa baadhi ya waumini wa madhehebu mengine wanaziona itikadi zenu zinatofautiana kidogo na za kwao na wakati mwingine kukubezeni. Hata hivyo mmekuwa mkihubiri kwa subira, upendo na uvumilivu huku mkizingatia ule usemi wenu maarufu wa “Love For All Hatred for None” yaani “Upendo kwa wote bila chuki kwa yeyote”


Swala la kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana miongoni mwa wanadini na waumini wa imani mbalimbali sio tu kwamba ni la muhimu bali ni la lazima katika nchi kama yetu na ulimwengu wa leo wa utandawazi kwa ujumla, kwani kwa bahati mbaya kwa kadri dunia inavyosonga mbele tunakabiliwa na tatizo kubwa la watu wenye misimamo mikali ya itikadi za kidini isiyokubali kuvumilia na kuheshimu imani wa wengine, tatizo ambalo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya uvunjifu wa amani duniani leo.


Aidha nimepata kufahamishwa kwamba sera ya Jumuiya yenu kama Jumuiya ya kidini duniani kote ni kutokujiingiza katika masuala ya kisiasa ya nchi yoyote, isipokuwa waumini wenu wanaweza kushiriki katika siasa za nchi zao katika ngazi ya mtu binafsi. Sera yenu hii ya kushughulikia masuala ya dini bila kuchanganya na siasa ni sera muhimu kwani ndiyo inayoweza kuhakikisha kwamba waumini wenu hawagawanyiki kwa misingi ya vyama vya siasa bali daima wanabaki kuwa kitu kimoja; Na jambo hilio nalo ni muhimu kwa ajili ya mandeleo ya Jumuiya husika na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Ninakupongezeni kwa msimamo huu na ninawaomba muendelee hivyo.

Mheshimiwa Amir,
Bila shaka nyote mnafahamu ya kuwa Serikali ya Tanzania haina dini, bali Watanzania ndio wenye imani mbalimbali za dini. Serikali ina wajibu wa kuziheshimu dini hizo kwa mujibu wa katiba ya nchi, na tunaamini kwamba jambo hili la kutoa uhuru wa dini/kuabudu limechangia sana katika amani ya nchi yetu. Mnajua kwamba ziko nchi duniani, dini fulani huonekana kuwa ndiyo dini ya taifa na kupewa haki zote na kuwaacha wenye imani zingine wakati mwingine wakiitwa ‘minorities’ wakinyimwa haki yao ya msingi ya kuamini na kuabudu sawa na uelewa wao. Ninakuhakikishieni kwmaba Serikali yenu Ya Tanzania itabaki na msimamo huu daima wa kuhakikisha kwamba kila mtanzania yuko huru kuamini na kuabudi jinsi apendavyo maadamu tu havunji sheria za nchi wala kusababisha shida kwa wengine.

Aidha Serikali inatambua mchango mkubwa ambao Jumuiya za kidini hutoa kwa jamii, mathalan huduma za maji, elimu, matibabu n.k. Jumuiya yenu haipo nyuma katika suala hili. Nimefahamishwa kwamba kwa takriban miaka mitatu sasa kupitia mradi wa “Water for Life” mumekuwa mkiendelea na uchimbaji na ukarabati wa visima vya maji safi katika maeneo ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro Dodoma na kwingineko.

Nimefurahishwa sana kusikia kwamba mnaendelea na ujenzi wa miskiti katika maeneo kadhaa ya vijiji vya Mkoa wetu wa Shinyanga na kwamba mwaka huu mnao mpango wa kuchimba visima vipatavyo 30 katika vijiji hivyo. Jambo hili litaongeza kasi ya maendeleo ya kielimu na kijamii katika vijiji hivi.

Mheshimiwa Amir,
Sisi tukiwa viongozi wa Serikali tunaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini waepukane na maovu mbalimbali mathalan utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi, rushwa, uzinzi (ambao hupelekea madhara mengi yakiwemo ugonjwa wa Ukimwi), uzururaji n.k. Bali dini hasa zinatufundisha kumuamini Mungu na kujiepusha na matendo ya ushirikina. Aidha kwa kuepuka tabia hizo mbaya jamii husonga mbele haraka kwenye maendeleo ya kiuchumi. Kwa ujumla iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wetu la 'Hapa kazi tu' kwani kila mtu ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.

Hivyo ni imani yangu kwamba Jumuiya yenu kama zilivyo taasisi zingine za kidini mnaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii yetu kwa kuwapatia waumini wenu na wananchi kwa ujumla elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho. Hapa kwenye mikoa yetu ya kanda hii kuna haja kubwa sana ya wananchi kupata elimu sahihi ya maadili kwani kuna matendo mengi yasiyo mazuri hasa ya ushirikina na mauwaji dhidi ya vikongwe.

Napenda niwahakikishieni kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za Jumuiya yenu an Jumuiya zingine  za kidini katika kupiga vita maovu ya kila aina.

Kama mnavyoelewa moja ya kipaumbele kikubwa cha Serikali yetu ni kupambana na ufisadi uliozagaa katika maisha yetu. Ufisadi huu ni kiashiria tosha cha hali yetu ya kimaadili ilivyo mbaya. Jumuiya na taasisi za kidini zinaweza kusaidia sana katika jambo hili iwapo zitaamua kupambana na ufisadi kutoka ndani mwao kwa kuwafahamisha waumini wao juu ya ubaya wa tabia hiyo chafu ambayo inapingwa na mfundisho ya dini zote.

Sawa na uelewa wangu hakuna dini ambayo inafundisha ufisadi, wizi, chuki, uhasama, dhuluma, uonevu na fujo, bali dini zote kwa njia moja au nyingine zinafundisha huruma, upendo, haki, uadilifu na kutendeana kwa wema kama ndugu.

Hivyo sote kwa pamoja tuhubiri maadili haya ili tuweze kujenga jamii ya Watanzania yenye kupendana, kuhurumiana, kuheshimiana na kusaidiana.

Mheshimiwa Amir na waumini wote

Mwisho; baada ya kusema hayo naomba tena niwashukuruni kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika mkutano wenu huu na ninawatakia heri na mafanikio. Yale yote mtakayokumbushana muweze kuyatekeleza.

Wasslaam.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم