Mwili wa Mchekeshaji nchini James Petro Nsemwa maarufu kwa jina la "Kinyambe" umezikwa juzi Jumamosi katika Makaburi ya Hayombe yaliyopo Uyole, Igawilo mkoani Mbeya.
Akizungumzia kuhusu nini kilisababisha kifo cha Kinyambe ,baba mzazi wa marehemu mzee Petro Lugendelo Nsemwa anaeleza....
"Marehemu alikuwa anaumwa kwa kipindi cha miezi nane, alikuwa anasumbuliwa na pafu la upande mmoja lilikuwa halipumui vizuri...kingine ambacho hufahamu ni kuwa ndani ya mwezi mmoja yaani siku kadhaa kabla ya Kinyambe kufariki alimpoteza mtoto wake wa mwisho Bray James Petro aliyekuwa na umri wa miaka minne, ila Mei 11 2016 ndiyo alifariki baba mtu yaani Kinyambe...
Jina halisi analotambulika katika familia yake ni James Petro Nsemwa na sio Mohammed Abdallah kama ambavyo wengi wanafahamu"
Mamia ya wakazi ya jiji la Mbeya walijitokeza kumzika aliyekuwa msanii wa vichekesho James Petro Nsemwa (30) maarufu kama Kinyambe ambaye alifariki dunia Jumatano ya wiki iliyopita mkoani Mbeya, katika makaburi ya Hayombe Uyole Igawilo mkoani Mbeya.
Msururu wa wakazi wa jiji la Mbeya pamoja na magari ulitembea kutoka nyumbani kwa wazazi eneo la Makondeko mtaa wa mtakuja kata ya Igawilo kuelekea makaburi ya bonde la uyole kwa umbali kilometa tatu na nusu.
Pia baadhi ya wasanii kutoka Dar es Salaam wakiongozwa na Kitale walihudhuria mazishi ya msanii mwenzao ingawa hapakuwepo na uwakilishi wa viongozi ngazi ya mkoa uliofika mazishini .
Msiba huo uliosimamisha shughuli mbalimbali kwa muda ili kupisha msururu wa watu na magari ambao ulikuwa ukielekea makaburini yaliyopo eneo la Nsalaga.
Baba wa marehemu, mzee Lugendelo Nsemwa, amesema kuwa akiwa nyumbani kwake Uyole, kuwa mwanaye ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa uchekeshaji, alianza kuumwa tangu Juni mwaka jana, ambapo moyo, tumbo na miguu ilikuwa imejaa maji pamoja na pafu la kushoto.
Alisema tatizo hilo lilipelekea mapafu yake kushindwa kufanya kazi sawasawa.
“Kwa kipindi kirefu alikuwa amelazwa katika hospitali mbalimbali kama vile Uyole, Ifisi, Rufaa na hospitali ya mkoa wa Mbeya, hali yake ilibadilika, alizidiwa na kupoteza fahamu, na bahati mbaya Jumatano saa 3 usiku akafariki dunia,” alisema mzazi huyo.
Mke wa marehemu
Komediani huyo aliyetamba kwa kubadilisha sura na sauti yake katika filamu za uchekeshaji nchini, James Petro Nsemwa a.k.a Kinyembe alizaliwa tarehe 19.09.1985 katika kijiji cha Mahanji- Matamba.
Kinyambe hakuwa na kiwango kikubwa cha elimu ambapo aliishia kidato cha pili mwaka 1999, kisha akajiunga na masomo ya sanaa katika mkoa wa Tanga kwa mwaka miwili.
Marehemu alikuwa msanii wa kuigiza na kuchekesha ambaye alizunguka mikoa karibu yote yaTanzania na nchi za nje kama vile Malawi, Msumbuji na Zambia.