Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumamosi tarehe 07 Mei, 2016 amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 586 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 waliomaliza mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Mkoani Arusha.
Maafisa hao wapya wa Jeshi walianza kozi yao tarehe 04 Mei, 2015 na wamepewa cheo cha Luteni usu.Kati ya maafisa wapya waliohitimu kozi yao leo, 80 ni madaktari na 6 ni marubani wa ndege waliopata mafunzo yao katika nchi tatu ambazo ni Tanzania, Uganda na Afrika Kusini.Kabla ya kutunuku Kamisheni kwa maafisa hao, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekagua gwaride la maafisa hao wapya na pia amepokea heshima ya gwaride lililopita mbele yake kwa mwendo wa pole na haraka, na baadaye kusikiliza ujumbe juu ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano, nidhamu ya kazi na uzalendo kupitia muziki wa bendi na kwaya.Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara nyingine amelazimika kuzungumza na wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa wamezuia msafara wake uliokuwa ukitoka Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kwenda Ikulu ndogo ya Arusha, na kuwahakikishia kuwa serikali yake imeanza kuwashughulikia wafanyabiashara ambao wameficha sukari kwa makusudi na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo.Rais Magufuli amesema tayari vyombo vya dola vimekamata tani 5,000 za sukari iliyofichwa na mfanyabiashara mmoja huko Tabata Jijini Dar es salaam na pia vimembaini mfanyabiashara mwingine aliyeficha sukari hiyo Jijini Arusha."Kweli nitawakomesha hawa, wasije wakanilaumu, haiwezekani ukaficha sukari wakati viwanda vyetu vinatengeneza sukari, kuna mmoja mwingine yupo Arusha hapa, nae ameficha sukari, alienda akanunua kwenye viwanda vya sukari vya hapa akaificha yote, leo ninamshughulikia."Kuna mwingine alinunua sukari pale Kilombero zaidi ya tani 3,000 akaficha, na mwingine ameshikwa pale Tabata alikuwa ameficha tani 5,000, na wanasubiri katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili ndugu zetu Waislamu wapate shida, haya ni mashetani makubwa, unawafichia watu chakula ambacho wanatakiwa kula, lakini nataka niwahakikishie ndugu zangu, hili ni tatizo la muda Tanzania, sukari itapatikana kwa wingi, na itanunuliwa na serikali, tumeshaagiza sukari lakini hatutawapa vibali hawa wafanyabiashara ambao wanatunyonya, tutanunua wenyewe na tutauza bei ya chini, hilo ndio lengo la serikali" Amesema Rais MagufuliAidha, Rais Magufuli amerejea kauli yake kuwa serikali yake haitawavumilia viongozi na watumishi wa umma ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, huku akisema ataendelea kutumbua majipu kwa yeyote atakayebainika kuchezea mali za umma ili kulinda maslai ya wengi, hususani watanzania wanyonge."Ninafanya kwa niaba yenu, ninafanya kwa niaba yenu, ningekuwa sifanyi kwa niaba yenu, na mimi ningeingia madarakani ningeanza kushirikiana na hao, na wengine walifikiria nitashirikiana nao, wamekwama mimi nitawatumbua kila siku ili Tanzania iwe ya neema iweze kwenda mbele, haiwezekani nchi kama hii tajiri, Tanzanite ipo, dhahabu ipo, wanyama mpaka nyani wameanza kuuzwa, wakimalizika nyani si tutauzwa na sisi ndugu zangu, ni lazima nisimamie hili" amesisitiza Dkt. Magufuli.Gerson MsigwaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULUArusha07 Mei, 2016Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akikagua gwaride kabla ya kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wapya 586 wa jeshi la Wananchi wa Tanzania kundi la 58/15 katika chuo cha kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha Mei 07,2016Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akitunuku kamisheni kwa maafisa wapya 586 wa jeshi la Wananchi wa Tanzania kundi la 58/15 katika chuo cha Mafunzo ya kijeshi cha Monduli TMA mkoani ArushaRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Afisa Mpya wa cheo cha Luteni Usu, Nasra Rashid ambaye alifanya vizuri zaidi kuliko Maafisa Wanafunzi wanawake katika chuo cha kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya wananchi General Davis Mwamunyange mara baada ya kuwasili kwenye chuo cha Mafunzo Kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akitembea kikakamavu mara baada ya kutoka kukagua gwaride katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi wa Ngarenaro waliomsimamisha wakati akitokea kwenye chuo cha Mafunzo ya Kijenshi cha Monduli mkoani Arusha.
Tags:
habari