Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli leo Jumamosi tarehe 07 Mei, 2016 amewatunuku Kamisheni Maafisa
wapya 586 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15
waliomaliza mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA)
Mkoani Arusha.
Maafisa hao wapya wa Jeshi walianza kozi yao tarehe 04 Mei, 2015 na wamepewa cheo cha Luteni usu.
Kati
ya maafisa wapya waliohitimu kozi yao leo, 80 ni madaktari na 6 ni
marubani wa ndege waliopata mafunzo yao katika nchi tatu ambazo ni
Tanzania, Uganda na Afrika Kusini.
Kabla
ya kutunuku Kamisheni kwa maafisa hao, Rais Dkt. John Pombe Magufuli
amekagua gwaride la maafisa hao wapya na pia amepokea heshima ya gwaride
lililopita mbele yake kwa mwendo wa pole na haraka, na baadaye
kusikiliza ujumbe juu ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano,
nidhamu ya kazi na uzalendo kupitia muziki wa bendi na kwaya.
Katika
hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kwa mara nyingine amelazimika kuzungumza na wananchi wa Arusha
Mjini waliokuwa wamezuia msafara wake uliokuwa ukitoka Chuo cha Mafunzo
ya Kijeshi Monduli kwenda Ikulu ndogo ya Arusha, na kuwahakikishia kuwa
serikali yake imeanza kuwashughulikia wafanyabiashara ambao wameficha
sukari kwa makusudi na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo.
Rais
Magufuli amesema tayari vyombo vya dola vimekamata tani 5,000 za sukari
iliyofichwa na mfanyabiashara mmoja huko Tabata Jijini Dar es salaam na
pia vimembaini mfanyabiashara mwingine aliyeficha sukari hiyo Jijini
Arusha.
"Kweli
nitawakomesha hawa, wasije wakanilaumu, haiwezekani ukaficha sukari
wakati viwanda vyetu vinatengeneza sukari, kuna mmoja mwingine yupo
Arusha hapa, nae ameficha sukari, alienda akanunua kwenye viwanda vya
sukari vya hapa akaificha yote, leo ninamshughulikia.
"Kuna
mwingine alinunua sukari pale Kilombero zaidi ya tani 3,000 akaficha,
na mwingine ameshikwa pale Tabata alikuwa ameficha tani 5,000, na
wanasubiri katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili ndugu zetu Waislamu
wapate shida, haya ni mashetani makubwa, unawafichia watu chakula
ambacho wanatakiwa kula, lakini nataka niwahakikishie ndugu zangu, hili
ni tatizo la muda Tanzania, sukari itapatikana kwa wingi, na itanunuliwa
na serikali, tumeshaagiza sukari lakini hatutawapa vibali hawa
wafanyabiashara ambao wanatunyonya, tutanunua wenyewe na tutauza bei ya
chini, hilo ndio lengo la serikali" Amesema Rais Magufuli
Aidha,
Rais Magufuli amerejea kauli yake kuwa serikali yake haitawavumilia
viongozi na watumishi wa umma ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo
vya rushwa na ufisadi, huku akisema ataendelea kutumbua majipu kwa
yeyote atakayebainika kuchezea mali za umma ili kulinda maslai ya wengi,
hususani watanzania wanyonge.
"Ninafanya
kwa niaba yenu, ninafanya kwa niaba yenu, ningekuwa sifanyi kwa niaba
yenu, na mimi ningeingia madarakani ningeanza kushirikiana na hao, na
wengine walifikiria nitashirikiana nao, wamekwama mimi nitawatumbua kila
siku ili Tanzania iwe ya neema iweze kwenda mbele, haiwezekani nchi
kama hii tajiri, Tanzanite ipo, dhahabu ipo, wanyama mpaka nyani
wameanza kuuzwa, wakimalizika nyani si tutauzwa na sisi ndugu zangu, ni
lazima nisimamie hili" amesisitiza Dkt. Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
07 Mei, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akikagua gwaride kabla ya kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wapya
586 wa jeshi la Wananchi wa Tanzania kundi la 58/15 katika chuo cha
kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha Mei 07,2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akitunuku kamisheni kwa maafisa wapya 586 wa jeshi la Wananchi
wa Tanzania kundi la 58/15 katika chuo cha Mafunzo ya kijeshi cha
Monduli TMA mkoani Arusha
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akimpongeza Afisa Mpya wa cheo cha Luteni Usu, Nasra Rashid
ambaye alifanya vizuri zaidi kuliko Maafisa Wanafunzi wanawake katika
chuo cha kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya wananchi General
Davis Mwamunyange mara baada ya kuwasili kwenye chuo cha Mafunzo Kijeshi
cha Monduli TMA mkoani Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akitembea kikakamavu mara baada ya kutoka kukagua gwaride
katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli TMA mkoani Arusha.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Dkt. John Pombe
Magufuli akiwasalimia wananchi wa Ngarenaro waliomsimamisha wakati
akitokea kwenye chuo cha Mafunzo ya Kijenshi cha Monduli mkoani Arusha.
Social Plugin