Watu wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti, akiwamo mtoto Mariam Haule (2) kwa kunyongwa na baba yake wa kambo baada ya kumtuma mama yake dukani kisha kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea Mei 2 mwaka huu.
Issa alisema kuwa mtuhumiwa huyo mkazi wa Kijiji cha Usimba, Wilaya ya Kaliua mkoani humo kabla ya kufanya mauaji hayo, alimtuma mkewe, Kalunde Malugu kwenda dukani kununua dawa .
Alisema baada ya mkewe kwenda dukani, alipata mwanya wa kufanya mauaji hayo kisha kutokomea kusikojulikana.
“Tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano ili tuweze kumkamata mtuhumiwa afikishwe kwenye mkondo wa sheria,” alisema Issa.
Kamanda huyo alisema jeshi hilo litahakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.
Mama wa mtoto huyo alisema alitumwa na mumewe dukani kununua dawa, lakini aliporudi alikuta mlango umefungwa na alipoingia ndani alibaini mtoto wake ameuawa.
Alisema hafahamu sababu za mauaji hayo na wala hakukuwa na malalamiko au madai yoyote kutoka kwa mumewe kuhusiana na mtoto huyo.
Katika tukio la pili; Mkazi wa Kijiji cha Rwamkoma wilayani Butiama, Magesa Machera (46) amekutwa ameuawa kwa kunyongwa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Mei 3, mwaka huu saa tisa usiku.
Alisema inadaiwa kuwa siku ya tukio hilo, mpenzi wake, Remmy Samwel (35) alitoka nje kwenda kujisaidia, lakini aliporudi alimkuta Machera akiwa chini amekufa.
Ng’anzi alisema mpenzi wake huyo ambaye ni mgeni katika kijiji hicho huwa na mazoea ya kwenda kumsalimia mara kwa mara na walikuwa wakinywa pombe za kienyeji. “Uchunguzi wa mauaji hayo unaendelea na polisi inamshikilia mpenzi wake,” alisema.