Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Limelaani Mauaji Ya Watu Watatu Msikitini Mwanza


Wakati Rais John Magufuli akitoa salamu za pole kwa wakazi wa jiji la Mwanza, kutokana na mauaji ya watu watatu waliouawa kwa kukatwa mapanga wakiwa msikitini, Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) limelaani mauaji hayo.


Aidha, Baraza hilo limewataka waislamu kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.


Kauli hiyo imetolewa na Mufti na Shehe Mkuu Abubakari Zubeir wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Jumatano saa mbili usiku wakati waumini hao wakifanya ibada.


Shehe Zubeir alisema tukio hilo la watu wasiojulikana kuvamia na kuwaua waumini msikitini ni la kinyama ambalo halipaswi kuvumiliwa.


“Kwa niaba ya Bakwata tunalaani vikali tukio hili pamoja na kuwataka waislamu kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu. Lakini pia nawaomba Waislamu na wananchi kwa ujumla kuvipa ushirikiano vyombo vyetu vya usalama ili wahalifu hawa wapatikane,” alisema Shehe Zubeir.


Alisema Uislamu ni dini ambayo moja ya misingi yake ni kulinda nafasi kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Kitabu Kitakatifu cha Quran na kuongeza baraza hilo linawapa pole wafiwa wote pamoja na waumini wa Masjid Rahmaan kwa msiba huo.


Aidha, alitoa agizo kwa Bakwata Mkoa wa Mwanza kufuatilia kwa karibu hali za majeruhi na wafiwa.


“Kama ambavyo naawagiza Bakwata Mkoa wa Mwanza nawaomba pia taasisi mbalimbali za Kiislamu pamoja na Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuwa tayari katika kusaidia familia za wafiwa kwani wanahitaji kufarijiwa na kusaidiwa,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post