Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mrisho Gambo amewaagiza Mganga Mkuu wa Wilaya pamoja na watumishi wa vituo vya afya vya wilaya hiyo kuacha kuwachangisha wananchi malipo ya huduma za afya zilizotangazwa kuwa zinatolewa bure.
Rai hiyo aliitoa hivi karibuni katika Kijiji cha Mazungwe kilichopo wilayani Uvinza wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho katika eneo la ujenzi wa Zahanati ya Kijiji unaoendelea wakati akiitambulisha kwa wadau wa maendeleo, lengo likiwa ni kuwaomba wadau hao waweze kuchangia ili kukamilisha ujenzi huo.
Gambo alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wanachangishwa kiasi cha shilingi 300 kwa kila mtoto na mama mjamzito anayehudhuria kliniki kwa kila mwezi hali inayosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuhudhuria kliniki pale wanapokuwa hawana pesa hiyo.
“Ni marufuku kwa Wilaya ya Uvinza kwenda kuwachangisha wananchi kwa huduma zilizotangazwa na serikali kuwa ni bure, na kama leo mngekuwa mmetozwa ningeamru hizo hela zirudishwe, ni vizuri huo mchezo wauache kwa sababu wengine watashindwa kupata huduma kwa kukosa shilingi 300” ,alisema Gambo.
Mganga mkuu wa Wilaya hiyo Fani Mussa alisema huduma zote zinatolewa bure na kwamba watumishi wanalipwa stahiki zao na kuwataka watumishi kuachana na tabia hiyo ya kuwatoza wananchi michango iliyokatazwa na serikali na kuahidi kulisimamia suala hilo.
Wakitoa malalamiko yao mbele ya mkuu wa wilaya hiyo,wananchi walisema wanasikitishwa na utaratibu wa wagonjwa kutozwa shilingi mia tatu ili waweze kupata huduma ya matibabu huku zahanati hiyo ikitoa huduma katika jengo bovu la nyasi pamoja na kukosa dawa, vifaa tiba na upungufu wa watumishi.
Walieleza kuwa watumishi hao wamekuwa wakiwatoza wagonjwa na hasa akina mama wajawazito wanaokwenda kliniki hali ambayo imesababisha baadhi ya wagonjwa kutokwenda kupata huduma katika zahanati hiyo na kwamba kutokana na zahanati hiyo kuwa na mapungufu wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata huduma katika kijiji jirani cha Kazuramimba.
Na Rhoda Ezekiel-Malunde1 blog Kigoma.
Social Plugin