TAASISI ya kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Katavi imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Diwani wa kupitia CCM Kata ya Katumba Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Senator Baraka Jerith kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa kiasi cha Tsh 400,000/= kutoka kwa mfugaji wa ng'ombe.
Mhumiwa huyo alifikishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa na kusomewa mashitaka mawili na wanasheria wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Simon Buchwa na Bahati Haule.
Mtuhumiwa anadaiwa kutenda makosa hayo mawili mnamo tarehe 12 Mei mwaka huu katika mgahawa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Ngandieta huko katika makazi ya wakimbizi ya Katumba kinyume na kifungu cha sheria 15 kidogo cha kwanza b cha sheria ya kudhibiti na kupambana na Rushwa Na 11 ya Mwaka 2011.
Siku hiyo mshitakiwa diwani alipokea kiasi cha shilingi laki nne kutoka kwa Mfugaji wa Ng'ombe anaitwa Charles Msukuma ili amsaidie kutohamisha mifugo yake kwenye eneo tengefu la makazi ya wakimbizi ya Katumba,na iwapo angekubali kumpatia kiasi cha shilingi milioni moja ili asitekeleze amri iliyotolewa na Mahakama ya mwanzo Katumba ya kumtaka mchungaji huyo kuondoa mifugo kwenye eneo hilo.
Wanasheria hao wa TAKUKURU walidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa katika shitaka la kwanza anatuhumiwa kwa kosa la kushawishi kwa nia ya kupokea rushwa kifungu cha 15 kidogo cha kwanza b cha sheria ya kupambana na rushwa Namba 11 cha mwaka 2011 sheria jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Shtaka la pili ni kosa la kupokea rushwa kiasi cha shilingi laki nne kinyume na sheria ambapo mshitakiwa baada ya kusomewa mashitaka hayo mawili alikana .
Mwanasheria wa TAKUKURU Simon Buchwa aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kesi hiyo kwa ajiri ya kutajwa kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo hauja kamilika .
Hakimu Mkazi Chiganga Ntengwa aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 30 na mshitakiwa alipelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya mdhamana ambapo alitakiwa kuwasilisha kiasi cha shilingi milioni mbili keshi mahakamani hapo au mali yoyote isiyo hamishika .
Mshitakiwa huyo ni miongoni mwa waliokuwa raia wa nchi ya Burundi ambao Serikali iliwapatia uraia wa Tanzania hivi karibuni.
Social Plugin