Familia ya Wilson Kabwe, aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, imesema ndugu yao alishawatoa wasiwasi kuhusu tuhuma zilizosababisha kusimamishwa kazi na Rais John Magufuli na kwamba alitamani uchunguzi ufanyike haraka ili ukweli ujulikane.
Kabwe aliyefariki dunia Mei 20 kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume jijini Dar es Salaam, alisimamishwa kazi na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni Aprili 19.
Miongoni mwa makosa yaliyosababisha kusimamishwa kwake ni madai ya kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo (UBT) Sh4000 na mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo mwaka 2009.
Kulikuwa pia na madai ya kukithiri kwa rushwa katika kituo hicho hasa katika kutoa magari na ukodishwaji wa vyumba vya kupangisha, kinyume na utaratibu na kuongeza muda wa mzabuni aliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya magari.
Akizungumza jana nyumbani kwao, Masaki jijini Dar es Salaam, mtoto wa marehemu, Joseph Kabwe alisema kifo cha baba yao hakikutokana na mshtuko wa kusimamishwa kazi, bali alianza kuugua muda mrefu na alishawaambia kuwa hana wasiwasi na tuhuma hizo, bali anataka uchunguzi ufanyike haraka.
“Alikuwa na saratani ya tezi dume na alikuwa akitumia dawa za chemotherapy ambazo ni kali sana na zilisababisha kuathirika kwa ini. Hata siku baba anatumbuliwa pale darajani alisema hana wasiwasi kwa sababu kila kitu kiko sawa sawa,” alisema Joseph.
“Baba alitutaka tusiwe na wasiwasi, tena mwenyewe alikuwa akisisitiza kuwa anatamani matokeo ya uchunguzi yatoke mapema ili ukweli ujulikane,” alisema.
Jana msibani kulikuwa na viongozi tofauti wa ngazi ya mkoa waliofika kutoa pole. Kaimu mkurugenzi wa jiji aliyekuwapo msibani hapo, Sarah Yohana alisema Halmashauri ya Jiji inashiriki msiba huo kwa kuwa Kabwe alikuwa mtumishi wao.
“Yule alikuwa mtumishi wa halmahsauri na ana haki zake kama mtumishi mwingine yoyote. Tutatoa jeneza, gari la kusafirishia maiti, chakula na rambirambi,” alisema Sarah.
Sarah alisema alikabidhiwa ofisi na Kabwe tangu Novemba mwaka jana baada ya kwenda kutibiwa nchini India. Kuhusu taratibu za utumishi, alisema licha ya Rais kumsimamisha kazi, hawakuwahi kuona barua yoyote iliyoletwa inayohusu kusimamishwa kwake.
“Inawezekana alipewa kwa njia nyingine, lakini sisi hatukuona barua ya kusimamishwa. Yule ni ‘presidential appointee’ (mteule wa Rais), yeye ndiye mwenye mamlaka na watu wake wa kufanya uchunguzi. Sisi hatujui, inawezekana wanafanya uchunguzi wao huko wenyewe,” alisema Sarah.
Jana Msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Eliab Mkenga Kabwe alisema hawana ugomvi wowote na Serikali huku akimkana mtu aliyejitambulisha kuwa msemaji wa familia hiyo, Dk. Zawadi Machuve aliyetoa maelezo kwa waandishi wa habari juzi kuwa hawataki viongozi wa Serikali wakanyage msibani.
Aliongeza kuwa familia hiyo inatambua na kuthamini mchango wa Serikali katika kugharamia matibabu na huduma zote za mazishi.
Alisema Makonda aliyetoa tuhuma za Kabwe kabla ya Rais Magufuli kutangaza kumsimamisha kazi, anatarajiwa kufika msibani hapo muda wowote.
“Mkuu wa Mkoa, Makonda bado hajafika hapa, lakini anaweza kufika wakati wowote. Unajua yeye ndiye mwenye mkoa wake kwa hiyo atafika tu wakati wowote,” alisema.
Mbali na viongozi wa jiji waliokuwapo kwenye msiba huo, viongozi wa mikoa mingine akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo na mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga walikuwapo msibani hapo.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, ambaye alikuwapo eneo hilo, ameshauri msiba huo uhamishiwe katika ukumbi wa Karimjee ikiwa ni kumpa heshima Kabwe aliyekuwa kiongozi wa jiji, lakini hakuna dalili za kufanya hivyo.