Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Yavunja Mkataba Na UDA




Hatimaye uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umevunja mkataba wa uwekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) na Kampuni ya Simon Group Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara, Robert Kisena.


Mkataba huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele ndani na nje ya Serikali, umetajwa kutokufuata taratibu za kisheria na kukiuka Sheria ya Manunuzi (PPRA).


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema uamuzi huo umefikiwa, baada ya kufanyika kikao halali cha Baraza la Madiwani.


Aidha baraza hilo la madiwani pia limeamua kwamba, asilimia 51 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni hiyo zirudishwe chini ya uongozi wa jiji hilo.


Mwita alisema madiwani walipitia upya mkataba wa uwekezaji kati ya kampuni hiyo na Halmashauri ya Jiji, ambapo walibaini udhaifu katika maeneo mbalimbali wakati wa makabidhiano.


Meya huyo anayetokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoshirikishwa wakati wa makabidhiano.


“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imevunja mkataba wa makubaliano ya kuuza Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa mfanyabiashara Robert Kisena, baada ya kubaini kuwapo udhaifu wakati wa kuuza shirika hili,” alisema.


Mwita alisema halmashauri ya jiji kipindi hicho, haikufuata utaratibu wa utangazaji wa zabuni wakati wa kuuza shirika hilo, hali iliyoonyesha wazi viongozi waliokuwa madarakani wakati huo, walikuwa na maslahi binafsi katika kukabidhi shirika hilo mikononi mwa kampuni hiyo.


Alisema hadi sasa shirika hilo bado limesajiliwa kwa jina la Halmashauri ya Jiji kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hali inayowapa nguvu ya kuvunja mkataba huo kwa sababu mmiliki wake kisheria bado ni jiji.


“Tuliambiwa Simon Group, alikuwa anakwenda benki kuchukua mikopo kwa hati ya Shirika la UDA, tumefuatilia benki mbalimbali tumebaini hakuna hata hati moja ya shirika iliyowasilishwa kwenye benki kama dhamana ya mikopo,”alisema.


Alisema shirika hilo hadi sasa lina Sh bilioni 5.9 ambazo zililipwa na Simon Group kama malipo halali ya kuuziana shirika, jambo ambalo haliko sawa.


“Hatuwezi kuona mikataba ya kifisadi inaendelea kuimaliza Serikali, lazima tuchukue hatua ambazo ni pamoja na kuangalia taratibu za kisheria ili kuivunja,’ alisema.


Alisema kutokana na hali hiyo, baraza hilo limeunda timu ya watu watatu wakiongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ili kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa kuvunjwa kwa mkataba huo.


Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Habari wa Kampuni ya Simon Group, Deus Bugaywa alisema hadi sasa halmashauri ya jiji haijatoa taarifa yoyote ya kuonesha kama mkataba huo umevunjwa, licha ya magari ya UDA kuanza kazi leo.


“Hatujapewa taarifa yoyote ambayo inasema mkataba kati ya UDA na Halmashauri ya Jiji umevunjwa, tunaamini bado ni wana hisa halali tutafanya kazi kwa ubia kama ulivyo mkataba wetu,”alisema Bugaywa.


Alisema kampuni hiyo, ilifuata taratibu zote za kisheria wakati wa kuingia makubaliano, wala hakukuwa na ukiukwaji wa kisheria.


Alisema kama watakabidhiwa barua ya kuvunjika kwa mkataba huo, wataangalia taratibu za kisheria ili waweze kudai haki yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post