Haya Hapa Matokeo ya Mchezo Wa Yanga Vs Sagrada Esperanca Huko Angola,Vurugu Yatokea Uwanjani,Kipa wa Yanga Apigwa Jiwe



 
Askari Polisi wakiwa uwanjani kutuliza vurugu leo



YANGA SC imefanikiwa kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji Sagrada Esperanca jioni ya leo Uwanja wa Esperanca mjini Dundo, Angola.

Kwa matokeo, hayo Yanga inakwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony. 

Matokeo hayo si tu yanamaanisha Yanga inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia yake, bali pia inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo ya michuano hivyo.

Awali ya hapo, Yanga imewahi kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ikafuatiwa na mahasimu, Simba SC mwaka 2003. 

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada El Moussa Nampiandraza, aliyesaidiwa na Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa wamekwishajipatia bao lao hilo.

Bao hilo lilifungwa na mkongwe Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama ‘Love Kabungula’ dakika ya 25, baada ya mabeki wa Yanga kufanya uzembe kidogo.

Yanga walitulia baada ya bao hilo, licha ya marefa kuonekana kabisa kupendelea wenyeji na wakafanikiwa kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nyuma kwa bao hilo moja tu.

Kipindi cha pili, Yanga waliachana na mchezo wa kujihamia na kufunguka kuanza kushambulia, hali ambayo ilipunguza kasi ya wapinzani wao.

Kocha Mholanzi alimtoa kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko baada ya kuumia na kumuingiza Deus Kaseke dakika ya 69.


Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 72.

Winga Simon Msuva alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 86 na dakika ya 89 kipa Deo Munishi 'Dida' akaokoa penalti iliyotolewa baada ya Nahodha, Cannavaro kumuangusha mchezaji wa Sagrada Esperanca. 

Refa aliongeza dakika tano baada ya kutimia dakika 90 na Nahodha Cannavaro akatolewa kwa kadi nyekundu pia dakika ya 90 na ushei.

Vurugu zikaibuka dakika ya mwisho ya dakika za nyongeza na kipa wa Yanga, Dida akapigwa jiwe na mchezo kusimama kwa muda.

 Askari Polisi waliingia uwanjani kutuliza fujo na mchezo ukaendelea kwa sekunde kadhaa kabla ya refa kumaliza.

Ikumbukwe, Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.

Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/Deus Kaseke dk69, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Kevin Yondan dk90 na Haruna Niyonzima.
 Na Prince Akbar-Angola

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post