Mfanyabiashara Naila Aminel (24) amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni tano baada ya kukiri kutumia mtandao wa kompyuta kutuma ujumbe wa lugha ya matusi.
Aminel ambaye ni mkazi wa Kariakoo, alihukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa.
Awali, akisoma mashitaka, Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 13 mwaka huu, maeneo ya katikati ya jiji, wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
Mitanto alidai kuwa mshitakiwa alitumia lugha ya matusi dhidi ya Martha Sebarua kupitia mtandao wa kompyuta kinyume na kifungu namba 23 (1) na (3) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Hata hivyo, Mitanto aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Mshitakiwa huyo alidai hakumtukana mlalamikaji isipokuwa alifanya hivyo kwa kuwa alimchukulia mume wake na walipiga picha za utupu na kumtumia kwenye simu yake.
Aliiomba pia mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana watoto wadogo ambao wanamtegemea.
Hakimu Mkasiwa alisema kuwa mshitakiwa amekiri kutumia lugha ya matusi hafai katika jamii na kwa sababu kosa lake ni la kwanza, atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni tano.