Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Kufanya Mkutano Mkubwa Wa Mwaka Mkoa wa Shinyanga ,Zaidi ya Watu 1500 Watakuwepo


Kiongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16,2016 katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga-SPC

Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga inatarajia kufanya mkutano wa Mwaka wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Shinyanga siku ya Jumapili wiki hii Mei 22,2016.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kuhusu maandalizi ya mkutano huo,kiongozi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza amesema mkutano huo utahudhuriwa na watu zaidi ya 1,500 kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.

Amesema lengo la mkutano huo wa mwaka ni kuhamasisha amani katika jamii kwa kuwakumbusha waumini kumjua mwenyezi mungu hali itakayosaidia kupunguza hata kumaliza kabisa vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji ya watu wasio na hatia kama vile vikongwe na albino.

“Lengo la mkutano ni kuwakumbusha waumini kuishi katika misingi ya kumfuata mwenyezi mungu,tunahitaji waumini washike mafundisho ili wawe raia wema,tunataka jamii iishi kwa amani”,anasema Luseza.

“Kila mwaka huwa tufanya mkutano wa mwaka,mwaka huu tutafanyia eneo la Nsalala kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga ambako kuna kituo chetu lakini pia kuna msikiti,tunarajia kukutana na waumini wetu kutoka maeneo mbalimbali ya ndani ya mkoa wa Shinyanga na nje ya mkoa wa Shinyanga”,anaeleza Luseza.

Luseza amesema mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga John Mongela na kuongeza kuwa viongozi mbalimbali wa serikali,viongozi wa Jumuiya hiyo akiwemo Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhiry watahudhuria mkutano huo .



Amesema kupitia mkutano huo, jamii itaelimishwa juu ya dhana potofu dhidi ya uislamu ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha dini hiyo pamoja na vikundi vya kigaidi mfano wa Boko haram, Isis, Al-shabaab na vingine vingi.



“Ukweli upo wazi dini ya kiislamu misingi yake mikuu ni amani na salama, na inapinga vikali suala la umwagaji wa damu ya mtu bila sababu, hivyo hawa wanaojiita na kuanzisha makundi ya ugaidi hapa duniani hawatokani na dini hii kwani mwenyezi mungu anaeleza wazi ndani ya kitabu chake cha kur-an kwamba, anayeua mtu mmoja ni sawa na kuua watu wote duniani”,ameeleza.



“Na yule anayemnusuru mtu mmoja ni sawa sawa na kuwanusuru watu wote duniani, kwa hali hii makundi haya yanayomwaga damu za watu wasio na hatia hayana uhusiano wowote na dini hii ya mwenyezi mungu, na wala yanachokifanya hakiwezi kuitwa jihadi ya kunusuru dini”, amesema Luseza.


Mkutano huo utaanza majira ya saa 3:30 asubuhi mpaka saa 9 alasiri katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga ambapo mada mbalimbali zinazolenga kuhamasisha amani zitajadiliwa.

Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya ina kiongozi mkuu duniani ambaye sasa anaitwa Khalifatul Masih v Hazrat Mirza Masroor Ahmad ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kujitahidi kuwaomba wanadamu kuishi kwa kuzingatia misingi ya amani.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post