Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Jumuiya Ya Wazazi CCM Mkoa wa Kigoma Yatoa Msaada Kwa Watoto Wanaosoma Katika Shule Maalumu Ya Walemavu Nengo Wilayani Kibondo

Viongozi wa Jumuiya ya wazazi wakikabidhi msaada kwa watoto wenye ulemavu katika shule ya Nengo wilaya ya Kibondo mkoa wa Kigoma-Picha na Rhoda Ezekiel -Malunde1 blog Kigoma



Katika kuadhimisha wiki ya wazazi mkoani Kigoma, Jumuiya ya wazazi CCM mkoani humo imetembelea shule ya msingi Nengo iliyopo Wilayani Kibondo (shule maalumu ya walemavu) mkoani Kigoma  kwa lengo ikiwa ni kujua changamtoto zinazowakabili ili waweze kuzitatua kama walezi.

Akizungumza shuleni hapo mgeni rasmi katika tukio hilo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Kigoma Nicholaus Zacharia alisema lengo kubwa la kufika shuleni hapo ni kutaka kujua changamoto zinazoikabili shule hiyo ili kuweza kuzitatua ikiwa ni kuonyesha umoja wao kwa vitendo kama walezi.

Katika ziara hiyo Zacharia alikabidhi msaada wa unga wa ugali, mchele, sukari, masufuria ya kupikia na baloo la nguo za mitumba ambavyo vinathamani ya fedha za kitanzania shilingi 1,200,000/= ambayo imechangwa na wanachama wa jumuiya hiyo kimkoa kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Muhambwe.

Akisoma taarifa ya shule hiyo mkuu wa shule ya msingi maalum Nengo Shabani Mzenzi aliwapongeza wazazi hao kwa kukumbuka watoto na kusema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 616 ambapo wanafunzi 81 ni walemavu na 535 ni wanafunzi wa kawaida.

Alisema walemavu hao ni pamoja na walemavu wa ngozi, wasiioona, wasiosikia pamoja na wenye mtindio wa ubongo na kusema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya kufundishia watoto wenye ulemavu, upungufu wa mabweni na ukosefu wa maji.


Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Muhambwe Mhandisi Atashasta Nditiye ambaye ni mlezi wa jumuiya hiyo mkoa alipokea changamoto hizo hizo na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi .
 Aidha alimuagiza mhandisi wa wilaya kufanya uthamini wa majengo yanayohitajika pamoja na mhandisi wa maji lengo kupata bajeti ili waweze kushirikiana na uongozi wa Wilaya kutatua changamoto hizo.

Alisema katika hatua za awali mbunge huyo ameshaandika maombi kwa wafadhili mbalimbali kuomba fedha za kutafuta changamoto ya vifaa vya kufundishia na kuomba bajeti aweze kutoa vifaa hivyo.


“Nimepokea changamoto zenu na ninaahidi kuzitafuta,mimi siyo mtaalamu hasa katika suala la vifaa ambapo naomba nipewe bajeti nianze kutekeleza kutatua changamoto hiyo, lakini pia katika miradi iliyotengwa kwa kila wilaya za mkoa wetu tutajitaidi kutoa ipaumbele kwa shule hii kwa kuwa ni ya wahitaji maalum” alisema Nditiye.


Naye katibu wa jumuiya hiyo Stanley Mkandawile alitoa wito kwa wazazi wote kuwa na moyo wa kusaidia watoto hao wenye uhitaji maalumu pamoja na wanaoishi mazingira magumu na kuwataka wazai kuzingatia uzazi wa mpango lengo kuzaa watoto wanaoweza kumudu mahitaji yao.

Na Rhoda Ezekiel-Malunde1 blog- Kigoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com