Chiza Dastan (31), anayesadikiwa kuwa mwizi wa pikipiki amefariki dunia Hospitali Wilaya ya Bukombe akipewa matibabu baada ya kupigwa na nyundo kichwani wakati akijaribu kupora pikipiki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema tukio hilo lilitokea Mei 20 saa 4.00 usiku nje ya Baa ya Geen View, Kata ya Katente wilayani Bukombe.
Mwabulambo alisema Chiza ambaye ni mkazi wa Kilimahewa, alifariki dunia wakati akitibiwa baada ya kujaribu kupora pikipiki ya Nassoro Tadeo aliyemkodi kutoka mjini Ushirombo kwenda kwenye baa hiyo.
Alisema wakiwa nje ya baa, ghafla mhalifu alianza kuongea na watu wasiojulikana kwenye simu, mwendesha bodaboda alishtuka na kutaka kuondoka.
Mwabulambo alisema wakati akijaribu kuondoka, Chiza alichomoa nyundo na kuanza kumshambulia mwendesha bodaboda na kumjeruhi kichwani.
Baada ya mwendesha bodaboda kupigwa nyundo kichwani, aliachia pikipiki na kuanza kupambana naye akig’ang’ania nyundo huku akiomba msaada.
Chiza alipanda pikipiki ili aondoke lakini mwendesha bodaboda, alifanikiwa kumnyang’anya nyundo na kuanza kumshambulia.
“Chiza alipoona kipigo kimezidi aliiachia pikipiki na kukimbia kusikojulikana, mwendesha pikipiki alichukua mali yake kwenda polisi ili kuandikiwa PF3 kwa ajili ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kupatiwa matibabu,” alisema.
Mwabulambo alisema mwendesha bodaboda kupewa PF na kwenda kutibiwa, akiwa hospitalini hapo alishtuka kuona Chiza akifikishwa na wasamaria wema saa 8.00 usiku akiwa na jeraha kubwa kichwani.
“Lakini kabla polisi hawajatoa PF3 walimhoji na kubaini kuwa, ndiye aliyejaribu kuiba pikipiki,” alisema Mwabulambo.
Hata hivyo, Mwabulambo ametoa wito kwa waendesha bodaboda kuwa makini wanapokuwa kwenye shughuli zao, hasa nyakati za usiku na kwamba wanapomhisi mtu watoe taarifa kituo chochote cha polisi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Mahona Kaji alisema majeruhi alipokelewa akiwa na hali mbaya kutokana na kupondwa na kitu kizito kichwani, fuvu la kichwa lilionekana limepasuka. Dk Kaji alisema walijitahidi kuokoa maisha yake lakini ikashindikana.