TAARIFA KWA WADAU WA HABARI MKOA WA SHINYANGA KUHUSU WATU WASIO WAANDISHI WA HABARI KUTUMIA JINA LA UANDISHI WA HABARI KWA MANUFAA YAO BINAFSI
Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club-SPC) inapenda kuwataarifu wadau wa habari mkoa wa Shinyanga kuwa makini na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidanganya kuwa ni waandishi wa habari wakati siyo waandishi wa habari.
Miongoni mwa watu wanaotumia majina ya vyombo vya habari kutapeli na kujipatia fedha ni Emmanuel Mpanda ambaye kwa nyakati tofauti amelalamikiwa na wadau wa habari pamoja na baadhi ya waandishi wa habari kuwa amekuwa akijiita mwandishi wa habari akitumia majina mbalimbali ya vyombo vya habari hasa Televisheni na kusababisha usumbufu pale wadau wanapohitaji kuona habari zao.
Klabu hii pia inafuatilia mienendo ya watu wengine wawili ambao pindi uchunguzi wetu utakapokamilika na kubaini udanganyifu wanaoufanya kwa wadau wa habari kwa kuwahadaa kuwa ni waandishi wa habari nao tutawaweka hadharani na kuviomba vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria.
Tunapenda kuwatahadharisha kuwa makini na watu wa namna hiyo ambao wanajiita waandishi wa habari wakati siyo waandishi wa habari kwani mbali na kuvichafulia majina vyombo vya habari pia wanashusha thamani taaluma ya Habari,huku wakitutia doa tunaohusika na tasnia hii kwa kuonekana sote hatufai.
Ili kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati muafaka tunaomba wadau wote wa habari muendelee kushirikiana na waandishi wa habari kwani jamii bila habari ni sawa na usiku wa giza.
Tunaomba wadau wa habari pale panapotokea shughuli ama tatizo lolote msisite kuwasiliana na ofisi ya Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kwa kufika moja kwa moja ofisini au kupitia mawasiliano yaliyopo hapo juu.
Tunatoa rai kwa waandishi wa habari kuwa na uchungu na taaluma yao na kutoruhusu tasnia ya habari kuchezewa kwa kuona haya kuwafichua Makanjanja ama kwa lugha nyingine “Waandishi wa Habari Hewa”,wanaodhalilisha taaluma hii.
Lakini pia hatutasita kuchukua hatua kwa waandishi wa habari wanaoshirikiana na waandishi hewa kwa shughuli za kiuandishi wa habari.
Tunaahidi kushirikiana na vyombo vya dola katika kuhakikisha kuwa taaluma ya uandishi wa habari inaheshimika.
Imetolewa na
Kadama Malunde
Mwenyekiti SPC
11.05.2016 |
Social Plugin