Rais John Magufuli ametoa mchango wa Sh. milioni 10 kwa ajili kusaidia matibabu ya mwanafunzi Bernadetha Msigwa aliyepata upofu hivi karibuni.
Msichana huyo anayesoma mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, ni miongoni wa wasichana ambao tatizo lake limeibuliwa kupitia kampeni ya Kipepeo, iliyoanzishwa na kampuni ya Clouds Media, Mei Mosi mwaka huu.
Kupitia matangazo yanayorushwa na kampuni hiyo, Rais Magufuli baada ya kusikia tatizo la Msigwa, ambaye pia picha yake imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwaomba Watanzania wamsaidie mchango wa fedha ili aweze kutibiwa. aliguswa na kuamua kutoa mchango huo.
Meneja wa kipindi cha 360 kinachorushwa kila siku za wiki asubuhi na televisheni ya Clouds, Hudson Kamoga alisema baada ya Rais kuona tangazo hilo, lililorushwa muda mfupi kabla ya kuanza uchambuzi wa magazeti, alimpigia simu.
“… Alisema ameguswa na stori ya Bernadetha, hivyo yeye na familia yake watachangia Sh10 milioni ili kumsadia,” alisema Kamoga.
Kamoga ambaye aliwahi kupigiwa simu na Rais Magufuli akiwa katika ya kipindi hicho na kuwasifu yeye na wenzake wanaokiendesha, alisema baada ya muda mfupi, Rais alimwagiza msaidizi wake apaleke mchango huo.
“Zilipita kama dakika 30 hivi au 45, akawa amemtuma mtu alete zile hela,” alisema Kamoga.
Mbali na Rais Magufuli, Kamoga alisema viongozi wengine walioguswa na tatizo la Msigwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye alikuwa mgeni kwenye kipindi cha 360 jana asubuhi, alichangia Sh2 milioni.
Pia, Manaibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Anthony Mavunde Dk Abdallah Posi kila mmoja alichangia Sh1 milioni na Mkurugenzi wa Kampuni ya TSN, Farough Baghozah alichangia Sh3 milioni.
Kamoga alisema mwitikio wa Watanzania umekuwa mkubwa na hadi jana, michango iliyokuwa imetolewa ilikuwa zaidi ya Sh30 milioni anazohitaji Msigwa kwa ajili ya matibabu.
Kamoga alieleza kuwa msichana huyo alianza kupata maumivu makali ya kichwa mwaka huu na baada ya muda, alipoteza uwezo wa kuona.
“Hakuzaliwa kipofu. Amepata tatizo mwaka huu, wakiwa chuo mwaka wa tatu,” alisema Kamoga.
Alisema aliomba msaada kwao hivyo kupitia kampeni ya kipepeo, tatizo lake limefahamika na wengi na Watanzania wamemchangia ili aweze kutibiwa na kuona tena.