Baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kuahirisha kumhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, hatimaye hatua hiyo sasa imeelekea kutekelezwa.
Taarifa rasmi ya jeshi hilo visiwani Zanzibar, imemtaka Maalim Seif afike katika Ofisi za Makao Makuu ya Polisi, Ziwani mjini hapa leo saa 4.00 asubuhi.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa CUF, Salim Bimani alithibitisha Maalim Seif kupokea barua hiyo jana wakati akiwa njiani kuelekea Dunga, Wilaya ya Kati Unguja, akiendelea na ziara yake katika majimbo ya Unguja.
“Ni kweli Maalim amepokea taarifa hiyo na ametakiwa afike Ziwani (mjini hapa) kesho (leo) saa nne asubuhi,” alisema Bimani
Bimani aliongeza kuwa hatua hiyo ya sasa imekuja baada ya jeshi hilo kuahirisha hatua ya wito wa kumhoji Maalim Seif, Ijumaa iliyopita.
Barua hiyo ya kuahirisha iliyosainiwa na Msangi kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar Mei 26, yenye kumbukumbu namba PHQ/ Z/C.5/4/4/TEMP/34 kwenda kwa Maalim Seif ilikuwa na kichwa cha habari ‘Kuahirisha mahojiano’.
“Tafadhali rejea barua yangu PHQ/Z/C.5/4/4/TEMP 26 ya tarehe 22/5/2016 ambapo tulikuita hapa Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kwa mahojiano maalumu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Ulinzi na Usalama wa Visiwa hivi,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Msangi.
Kadhalika, barua hiyo ya kuahirisha mahojiano hayo ilisema:
“Tutakujulisha mapema siku ile iliyosainiwa na DCP Salum ya mahojiano itakayofuata mara baada ya kukamilisha taratibu.”
Msangi alithibitisha wito huo wa leo baada ya hatua ya awali, kumtaka kiongozi huyo awasili mbele yao kwa mahojiano kama ambavyo walimuahidi awali.
Social Plugin