WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi sasa Serikali imekwishapokea maombi 52 kutoka makampuni mbalimbali ambayo yanataka kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini Tanzania.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia.
“Haya maombi yamekwishapokelewa na wenye makampuni wamekwishahojiwa kuangalia uwezo walionao katika suala zima la uwekezaji wanaotaka kuufanya, na tukiwapata wenye uwezo na wenye nia ya dhati watapatiwa miradi ya kuiendesha,” alisema.
Aliwataka Watanzania hao waishio Zambia watumie fursa ya uwepo wao huko kutafuta marafiki ambao wanaweza kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali nchini kwani Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu wakati wananchi wanahitaji kupatiwa huduma muhimu.
“Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi ya uwekezaji kwa hiyo tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo na ndiyo maana kule kwenye mkutano nimewaeleza washiriki kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi."
Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Alisema malengo ya Serikali ya awamu ya tano ni kuona kuwa nchi inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha umeme na umeme wote unaozalishwa na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi ya Taifa ili kuondokana na tatizo la mgao wa umeme nchini.
Alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati vikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo, nishati ya joto kutoka ardhini (geothermal energy) na nishati inayotokana na vinyesi vya mifugo (biomass) ambayo alisema vinatumika kwa watu wachache (siyo kitaifa).
Alisema kupatikana kwa gesi asilia nchini kumeleta neema ambapo mabomba ya gesi yamekwishajengwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka Kilwa-Songosongo hadi Dar es Salaam.
“Sasa hivi kuna utafiti unaendelea juu ya uwezekano wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani. Tumeanza pale Mikocheni (DSM) na sasa hivi wanafanya utafiti mwingine kule Mtwara ili wananchi waweze kutumia gesi hii kupikia badala ya mkaa,” alisema.
Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye makaa ya mawe, Waziri Mkuu alisema Serikali imelenga kutumia makaa ya mawe ili kuendeshea mitambo ya kwenye viwanda vikubwa badala ya kutumia umeme au mafuta ya dizeli kama inavyofanyika sasa.
“Baadhi ya wenye viwanda wanabadilisha mifumo ya kuendeshea mashine zao ili iweze kuendana na teknolojia ya makaa ya mawe pindi tu uchimbaji ukishika kasi,” alisema.
Akifafanua kuhusu juhudi za Serikali katika kusambaza nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji zaidi ya 3,000 katika ya vijiji 12,000 vilivyopo nchini vimefikiwa na nishati ya umeme.
“Tulianza na REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tunaenda awamu ya tatu. Hata mkipiga simu kwa ndugu zenu vijijini, mtakuta katika kila kata kuna vijiji kati ya vinne hadi vitano ambavyo vimefikiwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa REA,” alisema.
Waziri Mkuu amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).