Akiongea na East Afrika Television Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji mkoa wa Ilala, Mboje Kanga, amesema tukio hilo lilitokea jana usiku, na mpaka sasa hawajapata idadi kamili ya watu waliokuwa kwenye boti hiyo, wala mmiliki wake bado hajajulikana.
“Mpaka sasa hatuna taarifa rasmi ila tukio lilitokea usiku, ila ni kwamba kulikuwa na boti inavusha watu feri, na idadi kamili ya waliokuwa kwenye boti hilo haijapatikana, na hata kilichotokea rasmi bado hatujajua, ila kuna maiti mbili zimepatikana mmoja anaitwa Shangali Ibrahim Bimbwa, na mwengine anaitwa Thomas Beatus Nyoni, na kuna watu watatu inasemekana wameokolewa ila hatujawapata, inaonekana walikimbia baada ya tukio”, alisema Kamanda Mboje.
Kamanda Mboje amesema huenda watu hao walikimbia baada ya kugundua ni kosa kuvusha watu kwa boti katika eneo hilo, na mpaka sasa shughuli za uchunguzi zinaendelea sambamba na kutafuta miili ya watu wengine.
Chanzo-EATV
Social Plugin