Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Shirika la AGPAHI lakutana na Wafamasia na Waratibu Wa Maabara Mikoa ya Shinyanga na Simiyu,Angalia Picha Hapa


Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu limekutana na wafamasia na waratibu wa shughuli za maabara katika halmashauri za wilaya za mikoa hiyo katika kikao cha sita cha robo cha mwaka.


Kikao hicho cha siku mbili kimefanyika katika ukumbi wa Karena Hotel uliopo mjini Shinyanga,ambapo tarehe 05 Mei,2016 shirika hilo limekutana na wafamasia na wataalam wa maabara kutoka mkoa wa Simiyu na Mei 06,2016 likakutana na wafamasia na wataalam wa maabara kutoka mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza katika kikao hicho Mratibu wa Madawa na Mifumo ya Ugavi kutoka AGPAHI, Emilian Ng’wandu (pichani hapo juu) alisema lengo la kikao hicho cha sita cha kazi ni kupata taarifa kutoka katika halmashauri hizo kuhusu shughuli za usambazaji dawa na vifaa tiba katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma, kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili mafanikio na njia za kutatua changamoto zilizojitokeza wakati wa kutekeleza shughuli mbalimbali zihusuzo mfumo wa ugavi katika wilaya husika.

Ng'wandu alisema shirika la AGPAHI limekuwa likiratibu na kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa madawa ya magojwa nyemelezi na vitendanishi, mifumo ya ugavi, pamoja na kukutana na wadau wa afya katika mikoa hiyo sambamba na kushirikiana na serikali kupitia uongozi wa mkoa na wizara ya afya ili kuhakikisha kuwa watanzania wananufaika kupitia shirika hilo.

Ng’wandu aliongeza kuwa kutokana na juhudi mbalimbali katika kupambana na VVU na UKIMWI zinazofanywa na shirika la AGPAHI ,wamekuwa wakikutana na wataalam hao wa maabara na wafamasia, kila robo mwaka ili kuhakikisha kuwa huduma ya dawa na vifaa tiba vinapatikana katika vituo vya tiba na matunzo  katika vituo vyote vya afya ambako shirika linafanya kazi zake.


Awali akifungua kikao hicho ,Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Edgar Basheka alilishukuru shirika hilo kuwakutanisha wadau hao huku akitaja baadhi ya kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na shirika hilo kuwa ni kuwajengea uwezo wataalam wa afya,kusambaza dawa na vifaa tiba na vitendea kazi katika vituo vya afya pale inapohitajika.

Alisema kazi kubwa ya wafamasia na waratibu wa maabara katika wilaya na mikoa ni kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana katika vituo ,hivyo akawataka kufanya kazi kwa weledi huku wakitunza taarifa kila wanapotoa dawa na vifaa tiba.

“Naomba muache kufanya kazi kwa mazoea,msikubali kutoa dawa bila kujaza taarifa,ukikubali kudanganywa unaweza kuharibu kazi yako,niwakumbushe tu kwamba wananchi wanahitaji dawa na vipimo na wananchi waliolipia mifuko ya afya ya jamii ,wapeni huduma kama inavyotakiwa”,aliongeza Basheka.

Kwa Upande wake Meneja wa Miradi wa AGPAHI wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu  Dr. Gastor Njau ,alisema shirika lake limekuwa likisaidia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya hasa vile vya Tiba na Matunzo kwa Watu Wanaoishi na VVU pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika vituo hivyo.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Mshauri wa Maabara kutoka Mpango wa taifa wa Kudhibiti UKIMWI Selestine Kato,Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Edgar Basheka, kwa niaba ya Mfamasia mkuu wa serikali na Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa(MSD) Kanda ya ziwa Victor Sungusia.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mkurugenzi wa Timu ya Washauri wa Mifumo ya Ugavi wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Ondo Baraka na maafisa mbalimbali kutoka shirika la AGPAHI.

Mwandishi Mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde,ametuletea picha za kikao hicho siku ya kwanza kwa washiriki kutoka mkoa wa Simiyu na siku ya pili kwa washiriki kutoka mkoa wa Shinyanga,Angalia hapa chini


SIKU YA KWANZA-Mratibu wa Madawa na Mifumo ya Ugavi kutoka AGPAHI, Emilian Ng’wandu akiwakaribisha wafamasia na waratibu wa maabara kutoka mkoa wa Simiyu katika kikao hicho cha kazi ambacho alisema kinalenga kuboresha shughuli za usambazaji na upatikanaji wa dawa na kuboresha huduma ya maabara katika vituo vya vilivyopo katika halmashauri za wilaya za mkoa wa Simiyu

Ng’wandu alisema Shirika la AGPAHI limekuwa likiratibu vikao mbalimbali vya wataalam wa afya ili kuhakikisha kuwa huduma afya zinaboreshwa katika vituo vya afya. Alisema kikao hicho kinacholenga kubadilishana uzoefu kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushirikiano miongoni mwa wadau hao katika kutoa huduma ya afya.

Meneja wa Miradi wa AGPAHI wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu Dr. Gastor Njau akieleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI

Meneja wa Miradi wa AGPAHI wa mikoa ya Shinyanga na Simiyu  Dr. Gastor Njau akisisitiza jambo

Mratibu wa Madawa na Mifumo ya Ugavi kutoka AGPAHI, Emilian Ng’wandu akimkaribisha Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Edgar Basheka

Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Edgar Basheka,aliyemwakilisha mfamasia mkuu wa serikali ,akifungua kikao hicho ambapo alilishukuru shirika hilo kuwakutanisha wadau hao huku akitaja baadhi ya kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa afya,kusambaza dawa na vifaa tiba na vitendea kazi katika vituo vya afya.
 
Dr. Njau (kulia) na Mkurugenzi wa Timu ya Washauri wa Mifumo ya Ugavi wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto, Ondo Baraka wakifurahia jambo ukumbini
Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto, Edgar Basheka alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wafamasia na waratibu wa maabara katika wilaya na mikoa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri
Basheka aliwasisitiza baadhi ya wakuu wa vituo pale wanapoondoka vituoni wawe wanakabidhi vituo kwa watu wengine kwani baadhi yao wanaposafiri huondoka na funguo za ofisi na kusababisha usumbufu kwa wagonjwa wanaofika kituoni kupata huduma za afya
Mtaalam wa Mifumo ya Ugavi na Afya ya Jamii kutoka wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Edgar Basheka(wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati wa majadiliano,wa kwanza kushoto ni Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kanda ya Ziwa Victor Sungusia 
Washiriki wa kikao hicho wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini

Mratibu wa Shughuli za Maabara wa wilaya ya Maswa Iddi Yahya Hoza,ambaye pia ni afisa Viwango Maabara hospitali ya wilaya ya Maswa akitoa taarifa ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa.
Mkurugenzi wa Timu ya Washauri wa Mifumo ya Ugavi wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia ,wazee na watoto Ondo Baraka, akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema AGPAHI imekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI huku akiyataka mashirika mengine kuwa karibu na AGPAHI ili wajifunze namna shirika hilo lilivyofanikiwa .

“AGPAHI imekuwa ikitoa misaada ya kugharimia shughuli mbalimbali na kuwapa elimu wataalam wa afya katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu,ni ukweli usiopingika kuwa mabadiliko makubwa yamepatikana katika sekta ya afya nchini tunaomba tuungane nao katika mapambano haya dhidi ya VVU na UKIMWI”,alieleza Baraka.
Meneja wa MSD Kanda ya Ziwa Victor Sungusia akizungumza katika kikao hicho ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wataalam hao maabara na ugavi kuwasiliana na MSD pale wanapoona kuna tatizo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata dawa na vifaa tiba kama inavyotakiwa.

Mshauri wa Maabara kutoka Mpango wa taifa wa Kudhibiti UKIMWI(NACP) Selestine Kato akiwasilisha taarifa yake, ambapo pamoja na mambo mengine alisema wamekuwa wakishirikiana na shirika la AGPAHI kuboresha huduma za Watu Wanaoishi na VVU (WAVIU) huku akisisitiza kuwa shirika hilo limekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa watoto na jamii kwa ujumla.
Mshauri wa Maabara kutoka Mpango wa taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP)Selestine Kato akiwasilisha taarifa yake

Mwakilishi wa Halmashauri ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, mfamasia wa wilaya Bw. Kambona akitoa taarifa ya wilaya yake
SIKI YA PILI- Mwenyekiti wa kikao hicho, mfamasia wa mkoa wa Shinyanga, John Mfutakamba akieleza jambo kabla ya kumkaribisha mwakilishi kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, wazee, jinsia na watoto, Edgar Basheka kwa ufunguzi wa kikao.

Mshauri wa Maabara kutoka Mpango wa taifa wa Kudhibiti UKIMWI(NACP) Selestine Kato akizungumza katika kikao hicho, ambapo alisema pamoja na kwamba AGPAHI imekuwa ikishirikiana na wizara ya afya kuitaarifu kama kuna shida katika vituo vya kutolea huduma huku wakisaidia katika kutatua changamoto hizo, ni vyema wafamasia na wataalamu wa maabara wakafanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi zaidi ili kupunguza changamoto hizo.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho

Mfamasia kutoka halmashauri ya Mji Kahama Shijo Beneth akiwasilisha taarifa ya wilaya yake

Mfamasia wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Hamza Seleman akiwasilisha taarifa ya manispaa ya Shinyanga
Kikao kinaendelea...katikati ni mratibu wa Maabara mkoa wa Shinyanga Muhdin Hamza

Picha ya pamoja wafamasia,waratibu wa maabara wa halmashauri za wilaya mkoa wa Simiyu, maafisa kutoka wizara ya afya, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi na AGPAHI

Picha ya pamoja wafamasia,waratibu wa maabara wa halmashauri za wilaya mkoa wa Shinyanga, maafisa kutoka wizara ya afya, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi na AGPAHI
Picha ya pamoja

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com