Miezi michache baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kukwaruzana na Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea chanzo kikiwa ni mgogoro wa Kiwanda cha Urafiki na kupelekana mahakamani, jana mabomu yalirindima kiwandani hapo wakati wafanyakazi wakiendeleza madai ya malimbikizo ya mishahara.
Awali, viongozi hao walifikishana mahakamani baada ya Kubenea kudaiwa kumtukana Makonda ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wakitatua moja ya migomo ya wafanyakazi hao.
Kubenea alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu nje na kutotakiwa kutoa lugha ya matusi kama alivyofanya kwa mkuu huyo, lakini madai ya wafanyakazi wa Urafiki bado hayajapata suluhu.
Katika vurugu hizo zilizoanza jana asubuhi askari mmoja alipigwa jiwe kichwani huku wafanyakazi watatu wakizirai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema vurugu hizo zilianza baada ya wafanyakazi hao kutoelewana.
“Waliokuwa tayari kuendelea na kazi walizuiwa na wenzao,” alisema Fuime.
Akizungumzia kuhusu askari kupigwa jiwe baada ya kuwasili eneo la tukio huku wafanyakazi watatu wakizirai alisema: “Wamepelekwa hospitali na tunawashikilia watu wanne.”
Mgomo huo ulianza mwishoni mwa mwaka jana wakati wafanyakazi hao wakidai stahiki ya mishahara na posho za usafiri, chakula na pango la nyumba.
Hukumu ya madai iliyotolewa Februari mwaka jana na Mahakama ya Kazi (CMA) iliagiza wafanyakazi hao zaidi ya 800 walipwe Sh4.5 bilioni kuanzia Aprili 30.
Jana wakati wakifuatilia utekelezaji wa hukumu hiyo, vurugu zilitokea huku magari zaidi ya 10 yaliyosheheni askari yakiwasili eneo la kiwanda hicho na kufanikiwa kutuliza vurugu hizo.
Meneja Rasilimali Watu wa kiwanda hicho, Dickson Machilika alisema uongozi upo tayari kuwalipa stahiki zao, lakini umepanga kulipa kwa awamu.
Alisema uzalishaji wa kiwanda umeshuka na hata wafanyakazi wanaingia mara moja tofauti na awali kulipokuwa na awamu tatu.
Wakati huohuo, Wafanyakazi wa Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi (SBC) jana waligoma wakishinikiza uongozi wao kuwapa mikataba ya kuongezewa mishahara.
Katika mgomo huo, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi hao ambao walikuwa mbele ya lango la kampuni hiyo wakiimba.
Wafanyakazi hao waliilaumu kampuni hiyo kwa kumpa wakala jukumu la kuajiri na kulipa mishahara yao jambo linalosababisha ucheleweshwaji wa malipo.
“Wakala hatumtaki na kwa nini kampuni kubwa kama hii badala ya kuajiri watu, wanawapa mawakala na kusababisha sisi kutolipwa haki zetu,” alisema Dunia Shabani.
Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Irenus Mushongi alisema anashangaa kitendo hicho kwani walifanya mazungumzo na wafanyakazi hao na walikuwa katika hatua za kutafuta ufumbuzi.
“Mipangilio ipo tena kwa mujibu wa sheria nashangaa kabla ya makubaliano wamelianzisha,” alisema.
Ofisa Kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira, Omari Sama alisema madai hayo yalifikishwa wizarani na kujadiliana na pande zote na kutoa muda kwa mwajiri kutekeleza madai yao ndani ya siku 30.
Social Plugin