Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Polisi Waua Majambazi Wawili Mkoani Mwanza


Watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi mkoani Mwanza baada ya kurushiana risasi na askari wakati wakiwa kwenye harakati za za kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara wa madini, Baraka Said.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Augustino Senga alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita saa 5:30 usiku katika Mtaa wa Kigala Kata ya Buswelu Wilaya ya Ilemela. Alisema katika tukio hilo polisi walikamata silaha moja na risasi 21.


Senga alisema majambazi hao waliokuwa wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 na 45 hawajafahamika majina wala makazi yao.


“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuwapo kwa majambazi yanayokusudia kuvamia kwa mfanyabiashara huyo, tuliweka mtego eneo la tukio ndipo majambazi hayo yalikuja yakiwa kwenye gari jeusi majira ya saa tano usiku,” alisema Senga.


Katika tukio jingine, Wakazi wa stendi mpya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Daudi Joseph (32) na Magashi Mzee wameuawa kwa kupigwa mawe na fimbo na wananchi baada ya kudaiwa kuwatapeli wafanyabiashara wa ng’ombe.


Tukio hilo lilitokea Mei 5, saa saba mchana katika mnada wa mifugo uliopo Kijiji cha Maligisu wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza.


Senga alisema walichukua fedha kwa wafanyabiashara hao wa mifugo wakidai kuwauzia ng’ombe, lakini badala yake walitokomea pasipo kufanya hivyo.


Wakati huohuo, watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi wamevamia duka na kupora fedha ambazo haijajulikana kiasi chake.


Senga alisema tukio hilo lilitokea katika Kata ya Kishiri, wilayani Nyamagana.


Alisema watu hao walivamia duka hilo linalomilikiwa na Phares Grabriel (56).


Senga alisema pia walivamia duka la jirani la Revocatus Phares(28) na kuiba kompyuta mpakato, simu moja na kutokomea na pikipiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com