Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza bajeti ya Serikali hiyo ya Sh bilioni 841.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017; na kupandisha mshahara kwa kima cha chini kutoka Sh 150,000 hadi Sh 300,000.
Hatua hiyo imelenga kuongeza ufanisi na kupambana na ugumu wa maisha kwa wafanyakazi wake, kubana matumizi ya ndani na kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Khalid Salum Mohamed ndiye aliwasilisha bajeti hiyo katika Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.
Alisema vipaumbele katika bajeti hiyo ni katika kuimarisha sekta ya elimu, afya na miundombinu ya bandari na uwanja wa ndege.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakadiria kutumia Sh bilioni 841.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 445.6 kwa kazi za kawaida na Sh bilioni 395.9 kwa kazi za maendeleo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2016-2017 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo katika mchakato wa kukamilisha na kuanza kwa miradi miwili mikubwa ya miundombinu, ambayo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume katika jengo la abiria.
Aidha alisema ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mpigaduri, utasaidia kuongeza mapato na ajira kwa wananchi wa Zanzibar mara utakapomalizika.
Dk Salum alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kupungua kwa fedha kutoka kwa washiriki wa maendeleo; na ndiyo maana bajeti hiyo itajikita zaidi katika kuweka kipaumbele cha makusanyo ya kodi ya ndani.
“Tumeweka kipaumbele zaidi katika makusanyo ya kodi kupitia vyanzo vyake, ambapo taasisi za ukusanyaji kodi Mamlaka ya Mapato (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) tumezipa majukumu makubwa zaidi katika makusanyo ya kodi,” alisema Dk Salum.
Alifahamisha kwamba TRA inatarajiwa kukusanya Sh bilioni 188.8, wakati ZRB itakusanya Sh bilioni 237.4. Waziri huyo alisema muelekeo wa uchumi wa Zanzibar ni kufikia uchumi wa kati na usipungue asilimia nane kwa mwaka na kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Alisema SMZ imelenga Zanzibar kuwa nchi ya viwanda katika sekta ya kilimo na uvuvi na kuimarisha sekta ya utalii.
Aidha, alisema serikali imesikia kilio cha kupungiza kodi ya mishahara ya wafanyakazi zaidi kipato cha chini, ambapo sasa kitapunguzwa kutoka asilimia 13 hadi 9.
Salum alitangaza kwamba katika bajeti ya fedha kwa mwaka 2016-2017, hakutakuwa na ongezeko la kodi kwa lengo la kupunguza mzigo kwa wananchi.