Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vilivyomo ndani ya wizara hiyo, ikiwemo Jeshi la Polisi ili kupitia upya utaratibu wa kutoa ajira na kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliyetaka kufahamu ni kwa nini Serikali inasitisha ajira katika Jeshi la Polisi, wakati bado nchi inakabiliwa na uhaba wa askari ndani ya jeshi hilo wakiwemo askari wa kike.
“Tumesitisha kutoa ajira ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo chini ya wizara hiyo,” alisisitiza.
Miongoni mwa vyombo hivyo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mbali na Jeshi la Polisi ni Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uhamiaji.
Mbali na Komu, Mbunge mwingine ambaye ni wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema), alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua, ambapo pia alitaka kufahamu utaratibu wa uhakiki vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi umefikia wapi.
Akizungumzia Jeshi la Polisi, Masauni alisema Jeshi la Polisi limo kwenye utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache, wanaochafua taswira na kazi nzuri inayofanywa na Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwa kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili.
Kuhusu uhakiki wa vyeti, waziri huyo alielezea kuwa, uhakiki huo unahusu askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi unaendelea na mpaka sasa, askari 19 wamechukuliwa hatua za kisheria baada ya kugundulika kuwa walipata ajira kwa njia zisizokubalika.
Kuhusu uhaba wa askari wa kike, Waziri huyo alikiri kuwa kuna uhaba wa askari wa kike katika Jeshi la Polisi na kutoa mwito kwa wanawake wahamasike zaidi kujiunga na vyombo vya usalama.
Mwaka jana Idara ya Uhamiaji iliyokuwa chini ya Wizara hiyo, ililazimika kufuta ajira mpya 200 za makonstebo na makoplo, baada ya kubaini upatikanaji wa ajira hizo, ulifanyika kwa upendeleo.